NYERERE ALITAKA SERIKALI TATU

Wakati mjadala wa Katiba Mpya hususani muundo wa Muungano ukipamba moto, imebainika kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kupendekeza kuanzishwa Serikali ya Tanganyika, kama sharti la kuingia kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki.
 
Maelezo hayo ya Mwalimu Nyerere yapo kwenye kitabu chake cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania kilichoandikwa mwaka 1994 na kutolewa 1995.

 
“Wakati Mwalimu anaandika kitabu hiki mwaka 1994 taifa letu lilikuwa linakabiliwa na changamoto kadhaa za kihistoria ambazo ndizo zilimfanya kuingilia kati na kuandika kijitabu hiki ambacho kilikuwa kama nasaha, onyo, na usia kwa Watanzania,” inasema sehemu ya utangulizi wa kitabu hicho.

Katika sura ya nne ya kitabu hicho, pamoja na mambo mengine Mwalimu Nyerere alizungumzia suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo alieleza sababu zilizofanya muungano wa serikali mbili ukaanzishwa.

“Labda ni vizuri kukumbuka kwamba shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni kuziunganisha nchi za Afrika Mashariki ziwe nchi moja,” alisema katika kitabu chake hicho.

Alieleza kuwa, wakati Zanzibar na Tanganyika zinaungana, Kenya, Uganda na Tanganyika zilikuwa katika mazungumzo ya kutafuta uwezekano wa kuungana.

“Kama jambo hilo lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungekuwa ni wa shirikisho; ama shirikisho la nchi tatu zenye serikali nne, au shirikisho la nchi nne zenye serikali tano.

“Kwa kweli hata kesho nchi za Afrika Mashariki zikiamua kuungana na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye serikali mbili ya Zanzibar na ya Tanganyika kuliko Tanzania yenye serikali mbili, ya Tanzania na Zanzibar,” alisema.

Alisema kwa kufanya hivyo, wapendao Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa nchi moja, kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.

Baadhi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakizungumzia suala hilo, walisema kuwa ni vyema kuangalia zaidi matakwa ya wananchi kuliko kujali tu mfumo.

Mmoja wa wahadhiri hao, Faraja Christoms alisema wakati Mwalimu Nyerere akiandika kitabu cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania, alikuwa na hofu ya kumeguka kwa muungano.

“Wakati ule kulikuwa na wale wabunge wa G55 jina walilobatizwa na Profesa Issa Shivji, hawa wabunge walikuwa wanaona kama Zanzibar inapendelewa sana, walikuwa wanaona kama wanalalamika tu kama watoto.

“Lakini ukiwasikiliza na wenyewe Wazanzibari walikuwa na hoja, waliona kama Serikali ya Muungano ndiyo imekuwa ya Tanganyika kwa hiyo vitu vya Muungano vilikuwa vinainufaisha zaidi Tanganyika,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo ndiyo Mwalimu Nyerere alipoamua kuandika kitabu hicho.

Christoms alisema kwa mfumo wa sasa ulivyo ni vyema maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yakaheshimiwa, kwani hayatofautiani sana na yale ya tume nyingine zilizowahi kuundwa kuangalia suala la Muungano.

Alisema kwa kuwa tayari Zanzibar ina katiba yake ambayo imetambua visiwa hivyo kama nchi, siyo rahisi kubadilisha hali hiyo.

“Ukisema tuendelee na serikali mbili, kero za Wazanzibari hazitatatulika, ukitaka kulitatua hili kwanza useme haya mambo yasiyo ya Muungano nani ayashughulikie na yale ya Tanganyika pia yatashughulikiwa na nani?

“Mimi mwenyewe sioni kwa nini watu waseme tukiwa na serikali tatu muungano utavunjika kwa sababu muungano ni ridhaa ya watu, kwa sababu tayari Zanzibar ilishasema kuwa yenyewe ni nchi, Tume ya Warioba imebeba mawazo ya watu kwa hiyo ni vyema tukayaheshimu,” alisema Christoms.

Kwa upande wake Dk Aldin Mutembi alisema, “Mimi sijaingia ndani sana kwenye suala la serikali tatu ama mbili, lakini naungana na maoni ya Tume ya Warioba.”

Tume ya Warioba ilipendekeza kuwapo kwa serikali tatu.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Dk Wetengere Kitojo alisema kuwa, mawazo ya mwalimu yalikuwa serikali mbili kwa kuwa lengo lilikuwa katika kuelekea kwenye muungano wa serikali moja.

Alisema kwa sasa baadhi ya watu wanapiga kelele kutaka uwepo wa serikali mbili na wengine serikali tatu, ingawa ndani yake wapo ambao hawautaki kabisa muungano.

“Serikali mbili ni muungano bora zaidi, tumekuwa na mfumo huu kwa muda mrefu, lakini hatuoni kama kuna mwelekeo wa serikali moja, ndiyo maana watu wengine wameona bora tuwe na serikali tatu ili tupunguze kero ambazo zimeshindwa kutatuliwa kwa muda mrefu ndani ya mfumo wa serikali mbili.

“Mimi naona cha msingi ni nia ya dhati, wapo wanaotaka serikali mbili lakini hawana nia ya dhati ya muungano, wapo wengine serikali tatu lakini pia hawautaki muungano.

 Lengo ni muungano kamili, serikali tatu ni kurudi nyuma, ila sasa kama kwa miaka yote tumeshindwa kufikia lengo la serikali moja wengine wanaona bora turudi kwenye serikali tatu.


Alisema kuwa, kwa mtazamo wake serikali mbili ni bora zaidi ili baadaye iwepo moja lakini kama suala hilo limeshindikana ni bora kuwepo na mfumo wa serikali tatu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Emanuel Muya alisema mazingira yaliyomfanya Mwalimu Nyerere kuandika kitabu cha Uongozi Wetu Na Hatima ya Tanzania, ni tofauti na haya yaliyopo leo.

“Pamoja na yote bado kuna umuhimu wa kuungana Tanganyika na Zanzibar, hakuna anayetaka kuuvunja muungano, hata mwalimu alikuwa anataka muungano imara, alivyoondoka muungano ulikuwa imara.
“Uwe unakubalika pande zote, kwa sa
sa una matatizo pande zote, lazima tukubali kupata mazingira aliyokuwa akiyataka Mwalimu,” alisema.
Via>>MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post