KESI YA SHEIKH PONDA KUSIKILIZWA FEBRUARI 26


Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imesema itasikiliza maombi ya kufanya marejeo kuhusu kuliondoa shitaka la kukaidi amri halali iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam dhidi ya Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (pichani) Februari 26, mwaka huu.

Hatua hiyo  imefikiwa jana mahakamani hapo  baada ya Sheikh Ponda kuwasilisha upya maombi hayo kutokana na ya awali kufutwa na mahakama hiyo kwa kukosa mashiko ya kisheria.

Kesi hiyo iliahirishwa na Jaji Augustino Mwarija  baada ya upande wa Jamhuri kuomba  muda wa kujibu maombi ya mshtakiwa.

Kwa upande wake, Wakili wa utetezi, Nassoro Juma, alidai kuwa maombi ya Jamhuri hayana msingi wa kisheria kwa sababu walipokea nakala ya maombi hayo tangu Januari 22, mwaka huu hivyo ulikuwa na muda wa kutosha kuandaa majibu.

Juma alisema mshtakiwa yuko mahabusu tangu Agosti, mwaka 2013 bila sababu za msingi hivyo aliomba mahakama kutupilia mbali hoja za Jamhuri ili mshitakiwa apate haki yake.

Jaji Mwarija aliamuru upande wa Jamhuri kuwasilisha majibu Februari 24 na upande wa Utetezi kujibu Februari 25, mwaka huu na kesi hiyo itasikilizwa Februari 26, mwaka huu.


Katika kesi ya msingi, Sheikh Ponda anakabiliwa na mashtaka ya kukaidi amri halali, kuharibu imani za dini, kushawishi na kutenda kosa.
credit-Eddy blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post