Mauaji ya Shinyanga!! MKUU WA MKOA HUO ALLY NASSORO RUFUNGA AZUNGUMZA

Kulia ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga  ndugu  Ally Nassoro Rufunga,kushoto ni katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga ndugu Anselm Tarimo wakati wa kikao cha mkuu wa mkoa wa Shinyanga na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga
Kufuatia kuendelea kutokea kwa mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake mkoani Shinyanga  hususani katika wilaya ya Kahama na Kishapu mkuu wa mkoa huo Ally Nassoro Rufunga amelitaka jeshi la jadi sungusungu kushirikiana na serikali kuwabaini wahusika wa mauaji hayo kwani mara nyingi jamii ndiyo inawajua watu wanaofanya vitendo hivyo katika jamii kwa kisingizio cha imani za kishirikina.

Akizungumza juzi katika kikao chake na waandishi wa habari kuzungumzia fursa za uwekezaji na utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2010 katika mkoa wa Shinyanga kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2013 , kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi yake mkuu huyo wa mkoa alisema pamoja na serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi waachane na imani za kishirikina zinazopelea kutokea kwa mauaji lakini bado vitendo hivyo kutokana na jamii kutokuwa na hofu ya mungu.

“Jamii imekosa elimu dunia na elimu ahera,mtu umelala unaviziwa kisha kuuawa,wenye kuondoa tatizo hili ni wanajamii wenyewe kwani ndiyo wanawajua wauaji,sasa hivi tunawaandaa sungusungu,tutahakikisha sungusungu wanaimarishawa,hawa watatusaidia kuwabaini wahausika wa mauaji ya wenzetu wasio na hatia”,alisema  Rufunga.

“Tofauti na siku za nyuma,mauaji ya albino yamekwisha,na mauaji ya vikongwe yamepungua,mauaji yanayofanyika sasa ni mchanganyiko akina mama chini ya umri wa miaka 50 ndiyo wanauawa sasa,na sasa sisi serikali tunaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji haya”,aliongeza Rufunga.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza katika mkoa huo kwani suala la ulinzi limeimarishwa na linaridhisha lakini pia mkoa una vivutio vingi kwa wawekezaji kama vile mitandao yote ya mawasiliano ya simu kuwepo,usafiri wa reli,barabara na hata ndege,hali ya hewa nzuri,kuwepo kwa soko la ndani na nguvu kazi.

Aidha Rufunga alisema mkoa wa Shinyanga unatarajia kufungua viwanda vitano kabla ya mwezi Julai mwaka huu ambapo tayari wawekezaji wameshafanya majaribio ya mashine zao viwanda ambavyo vinatarajia kuwapatia  fursa za ajira kwa  wananchi zaidi ya elfu kumi .

Alivitaja viwanda hivyo kuwa ni kile  cha  maji na soda cha Jambo Group Company,kiwanda cha nyama na ngozi cha wachina kilichopo Ibadakuli,Kiwanda cha nyama cha Triple “S” kilichopo Old Shinyanga,Kiwanda cha mafuta ya kupikia(pamba na alzeti) cha wachina kilichopo eneo la Kizumbi na kiwanda cha kutengeneza nyuzi za kutengenezea nguo kinachojengwa na wawekezaji kutoka China kilichop Kizumbi mjini Shinyanga.

“Pamoja na kufunguliwa kwa viwanda hivyo pia bado kuna fursa nyingi za uwekezaji mkoani hapa mfano katika sekta ya kilimo tunahitaji wawekezaji hasa katika mazao ya biashara kama vile pamba,tumbaku na dengu,sekta zingine za uwekezaji ni  mifugo,utalii,maliasili,makazi,hoteli na ujenzo wa viwanda mbalimbali”,alisema Rufunga.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post