KAHAMA WAFUNGA MADUKA KAMA SHINYANGA MJINI LEO


Wafanyabiashara wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamefunga maduka kuunga mkono wenzao wa Shinyanga mjini Mwanza, Iringa, Mbeya na Dar Es Salaam ambao tayari wamefunga maduka yao huku wakimkataa Mwenyekiti wa TCCIA wilayani Kahama Bahati Matala.
Wafanyabiashara hao wamefunga maduka hayo kuanzia leo baada ya Uamuzi huo kutangazwa jana usiku na Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wilaya ya Kahama Simoni Mjika ikiwa ni sababu ya kupinga matumizi ya mashine za kutunzia na kutoa stakabadhi za mauzo (EFD).
Mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara wilaya ya Kahama Simoni Mjika akizungumza na wanachama wenzake waliofunga maduka yao
Mjika amesema wafanyabiashara wote kuanzia leo wamefunga maduka yote mpaka pale watakapopokea maelekezo mengine kwa wenzao wa Dar Es Salaam na Mwanza ambao wapo jijini Dar Es Salaam kwaajili ya mazungumzo na Serikali.

Aidha katika mkutano huo Wafanyabiashara hao wamekubaliana kwa pamoja kufunga biashara ya maduka yote yakiwemo ya Dawa Muhimu, mashine za kukoboa mpunga isipokuwa maduka ya kuuza nyama na masoko ya vyakula.

Kuhusu kumkataa Matala wafanyabiashara hao wamedai kuwa  ni kibaraka wa mamlaka ya mapato TRA ambaye hutumika kwa manufaa yao na maslahi yake binafsi huku wakimtuhumu nafasi hiyo aliipata kinyemela.

Kwa upande wake Matala amedai nafasi hiyo aliipata kihalali na wanaompinga si wanachama wa TCCIA ambao hawana sifa ya kuchagua au kuchaguliwa, ambapo  Katibu wa TCCIA Marcelina Saulo amesema wanapaswa kuwa wanachama hai ili wamkatae Mwenyekiti.  

Naye Mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya amewataka Wafanyabiashara hao wasifunge maduka kwani kufanya hivyo ni kuwakomoa wananchi wakati ambapo suala zima la matumizi ya mashine hizo ni elimu kutoka TRA.

Mpesya amesema TRA inapaswa kukaa nao meza moja na kuelimishana juu ya matumizi ya mashine hizo,ingawa mji wa Kahama hadi jana maduka yote yalikuwa yamefungwa huku idadi  kubwa ya Wateja wakiwa wanaranda randa madukani kutafuta huduma.

Credit-Dunia kiganjani blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post