DIWANI WA CCM ATUHUMIWA KWA WIZI WA MABATI YA MFUKO WA JIMBO YALIYOTOLEWA NA MBUNGE

Diwani wa kata Chigunga Hoja Mlyakalamu kupitia tiketi ya CCM anatuhumiwa kuiba mabati 14 kutoka katika mfuko wa jimbo uliotolewa na mbunge wa jimbo hilo mh, Lolecia Bukwimba katika jimbo la Busanda wilayani Geita na
ameamriwa ayarudishe ndani ya siku 14 baada ya kukiri jambo ambalo hadi sasa hajalitekeleza.

Tuhuma hizo zimefahamika mara baada ya mbunge huyo kutembelea shughuli za maendeleo katika jimbo lake na alipofika katika kijiji cha kayenze alipokuwa amesubiriwa kwa hamu tangu ubadhirifu huo utokee walimuueleza kwenye mkutano wa hadhara kuwa mabati uliyotoa katika shule ya msingi Sanza ni mangapi?

Taarifa kutoka kwa afisa mtendaji wa kata hiyo Bw William Mabilika alisema kuwa wao katika kikao cha maendeleo ya kata WDC walikaa na kuidhinisha kuwa mabati yakanunuliwe 100 ya geji 28 na muhtasari unasomeka hivyo na baada ya hapo wakamtuma diwani akiwa kama mwakilishi wa wananchi ili ayafuate mjini Geita waliponunulia.

Afisa mtendaji huyo alisema walishangaa kuona mabati 86 ya geji 30 tofauti na walivyokuwa wamekubaliana na inadaiwa kuwa waliyanunua kwenye duka la Kwilasa ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Geita.

Kwa upande wa mratibu elimu kata ya Chigunga Bw John Rugila amesema kuwa ni kweli walipewa sh milioni 2 na laki tano kwa ajili ya kununua mabati 100  katika shule ya msingi Sanza ili waezeke yenye geji 28 lakini ameshangaa kuona mabati 86 na geji 30.

 ‘’Ndugu mwandishi hata na mimi nashangaa kuona mabati pungufu tofauti na ilivyokubaliwa katika vikao vyetu vya WDC’’,alisema mratibu huyo wa kata.

Diwani huyo alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alikiri kwenda kinyume na makubaliano ya  kikao yeye akaleta mabati 86 badala ya 100 na yenye geji 30 badala ya 28 kama alivyoagizwa na WDC na kujitetea kuwa pesa zingine alitumia kwenye usafiri wa kuyasafirisha kutoka Geita hadi Kayenze.

 Aidha diwani huyo alipolizwa na waandishi wa habari kwamba  je hizo geji 30 badala ya 28 zimehusikaje katika gharama za usafiri,diwani huyo hakuwa na jibu.....akasema

“ Hata hivyo nimeamuriwa kuyarudisha mabati 14 tatizo lako ni nini? Alisema diwani huyo.
 Hata hivyo alivyoulizwa tena kwa vile anarudisha mabati 14 tu na geji 30 atayarudisha achukue geji 28? Alisema hana hela ziliisha.

Mbunge wa jimbo hilo Lolesia Bukwimba alisema amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwenye mkutano wa hadhara kwamba kuna upungufu wa mabati hayo na tofauti ya geji walizokubaliana  na kwamba diwani huyo alikiuka na hadi sasa shule hiyo haijajengwa.

 “Diwani huyo aliwahi kufanya mkutano hapo na kuwaambia ameleta mabati 86 kutoka kwa mbunge na 14 yaliyobaki atakuja nayo mbunge na ndipo nilipofika bila mabati wananchi wakaniuliza mabati yako wapi tuliyoambiwa na diwani utakuja nayo?”,aliongeza mbunge huyo

Kufuatia maswali hayo ya wananchi, mbunge alilazimika kutoa majibu kwamba yeye tayari alishatoa mabati 100 na yote yalishakuja wananchi wakamwambia kuwa aende na diwani wake na baada ya hapo mbunge huyo alimsimamisha diwani na kumuuliza kuhusu mabati hayo.


 ‘’Ndugu mwandishi niliagiza baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wanachi kwenye mkutano wa hadhara diwani alete hayo mabati ndani ya siku 14 kwani aliwadanganya hao wananchi na kunisingizia mimi kuwa nitakuja nayo mabati lakini hadi sasa hivi sijapata taarifa za kurudisha kwa mabati hayo’’ ,alisema mbunge huyo.
Na Valence Robert-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post