DAKTARI FEKI ATAHIRI WANAUMME 28 KWA NGUVU NYUMBANI KWAKE

NB-Picha haihusiani habari
Mtu anayedaiwa kujiita daktari mkazi wa Kijiji cha Mudio, Kata ya Masama Mashariki wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, (jina linahifadhiwa), anadaiwa kuwafanyia tohara kwa nguvu wanaume 28 nyumbani kwake akisaidiwa na kikundi cha vijana kinachomsaidia kuwakamata kwa nguvu wanaume ambao hawajatahiriwa. 


Habari ambazo zilizothibitishwa na watu mbalimbali akiwemo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dkt. Paul Chaote, daktari huyo bandia amekuwa wakiwafanyia tohara wanaume hao nyumbani kwake sebuleni. 


Mganga Mkuu huyo wa Wilaya ya Hai, Dkt. Chaote alithibitisha kuwepo kwa daktari huyo bandia, anayedai anafanya kazi katika hospitali moja kubwa iliyopo mkoani Arusha. 


Alisema madai ya daktari huyo kuwa anafanya kazi katika hospitali hiyo yalikuwa hayajathibitishwa.


Alisema tayari serikali imemzuia mtu huyo kuwafanyia tohara watu hao kutokana na kuwa daktari bandia. 

Habari ambazo zimethibitishwa na mmoja wa maofisa wa polisi ambaye hakutaka kutaja jina lake litajwe alithibitisha daktari huyo bandia kushikiliwa polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tuhuma hizo. 


Dkt. Chaote alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba daktari huyo bandia amekuwa akiwatibu wagonjwa wake hao kwa kutumia duka lake la dawa, lililopo kijijini hapo licha ya kwamba halitambuliki na mhudumu wake hana sifa. 


“Tulipata taarifa kuhusu kufanyiwa tohara kwa wanaume wa kijiji cha Modio na baada ya kufuatilia tulibaini ni kweli na tulipomhoji, (daktari bandia) alidai ni daktari msaidizi katika hospitali iliyopo mkoani Arusha. 


Alisema baada ya taarifa za tukio hilo walifuatilia kijijini hapo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na kubaini nyumba na vifaa vilivyokuwa vikitumika kufanya tohara.


Alisema vifaa alivyokuwa akitumia havikubaliki kiafya. 

“Tumeanza uchunguzi ili kupata watu waliofanyiwa tohara ili kujua wanaendeleaje kiafya, hii ni kutokana na aina ya huduma aliyokuwa akiwapa kuwa haikubaliki kiafya,” alisema. 


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masama Mashariki, Ally Mwanga, alikiri kutokea kwa tukio hilo akisema limesababisha usumbufu kwa wananchi, huku wengine wakishindwa kwenda katika shughuli za uzalishaji mali kwa hofu ya kukamatwa na vijana na daktari huyo bandia ili wakafanyiwe tohara. 


Mwanga alisema alipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi ya kufanyiwa vitendo hivyo na kutoa taarifa polisi wilayani Hai, ambapo baadaye uchunguzi ulifanyika na mhusika pamoja na timu yake kukamatwa.


Chanzo-Majira

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post