Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza mkakati wa kuwachukua waliokuwa viongozi wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Kahama waliofukuzwa uanachama hivi karibuni kwa
tuhuma mbalimbali ikiwemo kumuunga mkono aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama
hicho Mhe. Zitto Kabwe.
Katika mikakati hiyo katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa Bw. Sixtus Mapunda ameingia mjini
Kahama kimyakimya bila kuripoti sehemu yoyote na kufanya mkutano wa siri na
waliokuwa viongozi hao.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari kimedai kuwa Mapunda baada ya kufika mjini Kahama akitokea Dodoma amefikia
hotel mojawapo mjini humo kwa siri na kuwaalika baadhi ya makada wachache wa
CCM ambao amewapa masharti ya kutotoa taarifa yoyote juu ya ujio wake.
Mmoja wa watu aliowaalika
kwenye kikao cha awali kabla ya kukutana na makada hao wa CHADEMA amesema Katibu
Mkuu huyo hakutaka kujulikana kama ana mazungumzo na watu hao ingawa amefika
kwa kazi hiyo maalumu.
Hivi karibuni CHADEMA
kiliwafukuza viongozi wake sita wakiwemo watano wa Jimbo la Kahama, miongoni
mwao akiwa ni Diwani wa Kata ya Majengo Bw. Bobson Wambura, kwa madai ya kukiuka Katiba na
kuhujumu ya chama wakati wa uchaguzi mdogo wa Udiwani wa Kata ya Ubagwe uliomalizika hivi karibuni .
Wambura ambaye pia alikuwa
Katibu Mwenezi wa Jimbo alifukuzwa sambamba na Mwenyekiti wa Jimbo la
Kahama Bw. Israel Barakiel, Katibu wa Jimbo hilo Bw. Vicent Kwilukilwa, Mwenyekiti wa
BAVICHA Jimbo Bw. Benedicto Shija, Mwenyekiti BAWACHA Jimbo Bw.Kasigwa Adram pamoja na
Mratibu wa Vijana wilaya Bw. Vicent Manyambo.
Aidha katika kikao hicho
cha katibu mkuu wa UVCCM chanzo chetu kimeeleza kuwa waliokuwa makada hao wa CHADEMA wametakiwa kurudi CCM na katika
ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Bw. Abdurahman Kinana na Katibu Mwenezi wake Bw. Nape
Nnawiye inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni wilayani Kahama watakabidhi kadi za
CHADEMA.
Hata hivyo mazungumzo hayo
ya awali yameonesha kugonga mwamba baada ya kutofikia maelewano ya kimaslahi
kati ya Katibu huyo na wana CHADEMA hao waliofukuzwa ambapo mmoja wao aliyeongea kwa
niaba yao amesema wameshindwa kuelewana.
Mwana CHADEMA huyo
aliyefukuzwa Bw. Bobson Wambura kwa niaba ya wenzake amesema wameshindwa kuelewana
kutokana na kuwataka wajiunge kwanza na CCM na siku wakikabidhi kadi ndipo
watapewa fedha.
Pamoja na kuthibitika kuwa
Katibu Mkuu huyo wa UVCCM yuko mjini Kahama,lakini alipotakiwa kuthibitisha
kwa njia ya simu uwepo wake Bw. Mapunda amegoma akidai
hajawahi kufika Kahama kufanya kikao na watu hao,ingawa ameonesha kuwafahamu
wengine kwa majina.
Chanzo-Wangsteve blog