MBUNGE WA NZEGA DKT HAMIS KIGWANGALA ATISHIWA KUNYANG'ANYWA KADI YA UANACHAMA CCM

 

Habari kutoka mjini Nzega zinasema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nzega mkoani Tabora kinakusudia kumnyang’anya kadi mbunge wake, Dkt Hamisi Kigwangala baada ya kumtuhumu kwenda kinyume na matakwa ya chama hicho, pamoja na  kuwaadhibu  madiwani wake wanne baada ya madiwani hao hivi karibuni kuungana na mbunge huyo kufanya maandamano kupinga maamuzi ya baraza la madiwani kubadili matumizi ya fedha zilizotolewa na mgodi wa dhahabu wa Resolute Tanzania Ltd. kiasi cha shilingi bilioni 2.340 ikiwa ni ushuru wa huduma.


Dkt Kigwangala pamoja na madiwani hao wanne wanadaiwa kuungana na madiwani wengine wanaotokana na vyama vya CUF na CHADEMA pamoja na wakazi wa mji wa Nzega kufanya maandamano makubwa kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Nzega kumtaka azuie kutekelezwa kwa mabadiliko ya matumizi ya fedha hizo.

Imeelezwa kuwa kitendo cha Dkt. Kigwangala pamoja na madiwani kufanya mkutano wa hadhara na kisha kuandamana hadi kwa mkuu wa wilaya kiliwakera viongozi wa CCM wanaodaiwa kuwashinikiza madiwani kubadili matumizi ya fedha hizo na kuagiza zigawanywe katika kila kata badala ya kununulia mitambo ya kutengenezea barabara.

Hivi karibuni wananchi wa Nzega waliungana na mbunge wao na madiwani sita kuandamana kwenda kwa mkuu wa wilaya hiyo, Bituni Msangi kushinikiza azuie fedha hizo zisigawanywe katika kila kata kama walivyopendekeza madiwani mpaka muafaka utakapopatikana na kwamba kitendo cha kutengua bajeti ya awali kinapingana na utaratibu wa kanuni za halmashauri.

Wananchi hao walishangazwa na uamuzi wa madiwani kubadili matumizi ya fedha hizo ambazo tayari katika kikao halali kilichofanyika Aprili 24 na 25 mwaka jana kilipitisha bajeti ya matumizi yake na kuelekeza zinunulie mitambo ya kutengenezea barabara na ya kuchimbia visima vya maji na sehemu yake itumike kuanzishia benki ya watu wa Nzega.

Akiandika kupitia mtandao wake wa kijamii, mbunge wa Jimbo la Nzega, Dkt. Kigwangala alithibitisha kupata taarifa hizo ambapo hata hivyo alisema iwapo Chama chake kitachukua maamuzi hayo yuko radhi kuyapokea kwa vile sasa amechoka kuvutana na watu wasioitakia maendeleo ya kweli wilaya ya Nzega.

“Nimeshangazwa sana na kusikitishwa na jinsi Chama kinavyoendeshwa, ninaamini viongozi wakuu wa Chama wanafuatilia kwa ukaribu na watachukua hatua stahiki. Kwamba kuna watu wana nguvu kuliko Chama, kwamba wachache wanaweza kuwaonea wengine kwa kuwa wana vyeo na mamlaka ya kufanya hivyo, na hakuna wa kuingilia kati na kusema 'no',”

“Basi sina haja ya kuendelea kupambana. Nimechoka, sintokata rufaa wala sintolalamika tena! Watekeleze hukumu hiyo. Sintojitetea na sintohudhuria kikao chochote kile kuanzia sasa. Nimechoka kupambana na watu wenye nguvu, nimechoka. Ni bora kuwa mnyonge lakini ukabaki na uhai, uzima, heshima na furaha yako,” alieleza Dkt. Kigwangala.

Kwa upande wao baadhi ya madiwani wanaotuhumiwa kuungana na mbunge huyo kufanya mkutano na maandamano haramu ambayo pia yaliwahusisha madiwani wa vyama vya upinzani na viongozi wao wamekiri kupewa adhabu ya onyo kali kutokana na kitendo chao hicho.

“Ni kweli kabisa chama kimetuadhibu kwa kutupa adhabu ya onyo kali sisi madiwani wanne, ambapo hata wale waliokuwa na nyadhifa wamevuliwa nyadhifa zao akiwemo aliyekuwa katibu wa madiwani wa CCM, tumeonywa vikali sana tukidaiwa kushiriki maandamano na mkutano haramu, imetushangaza sana,”

“Lakini chanzo cha hali hii ni baada ya madiwani kuwagomea viongozi wa CCM ambao waliomba wapatiwe shilingi milioni 200 ili wajengee ukumbi wa mikutano utakaomilikiwa na chama hicho, lakini ukweli ni kwamba fedha hizo bajeti yake tuliishaipitisha tangu mwaka jana, tumekata rufaa mkoani kupinga adhabu hii,”

“Kwa kweli tuliona tukikubali ombi hilo lingeweza kututia matatani zaidi tulikataa kwa vile fedha hizo ni za wananchi wote wa Nzega na hazikutolewa kwa lengo ya kukisaidia  chama chochote cha siasa, nahisi tulipogoma ndipo tukashinikizwa tubadili matumizi ili sasa zielekezwe kwenye kata,” alieleza diwani huyo.

Hata hivyo kwa upande wake katibu wa CCM wilayani Nzega, Vyolohoka Kajolo akizungumza kupitia simu yake ya kiganjani hakuweza kukanusha moja kwa moja madai hayo ambapo aliwaomba waandishi kuwauliza madiwani wanaodai kuadhibiwa iwapo tayari wameishapatiwa barua zozote juu ya maamuzi hayo.

“Haya ni mambo ya ndani haturuhusiwi kuyatoa nje, hakuna mtu aliyeadhibiwa na kama ni kweli basi wawaonesha barua waliozopewa, na hatujamvua madaraka diwani ye yote yule wala kutishia kumpokonya kadi mbunge wetu, haya mambo hata mimi nimeyasoma kupitia mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari, hatujaadhibu mtu,” alieleza Kajolo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post