Majanga!! MAHINDI YA WANAFUNZI YACHAKACHULIWA KATA YA NDEMBEZI

Aliyesimama ni diwani wa kata ya Ndembezi pia naibu meya wa manispaa ya Shinyanga David Nkulila akiwa amepigwa bumbuazi baada ya kuangalia mahindi ndani ya gari lake ambayo yalionekana kuwa pungufu kiujazo baada ya kutolewa katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata ya Ndembezi mjini Shinyanga mapema leo tayari kwa ajili kusambaza katika shule tatu za msingi katika kata hiyo. Diwani huyo amesema kata ya Ndembezi hivi karibuni ilipata magunia 197 ya mahindi ya msaada kutoka ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa  yagawiwe kwa vijiji 19 vya kata hiyo kwa ajili ya kupunguza makali ya njaa.Katika magunia hayo 197,yeye binafsi kama diwani wa kata hiyo aliamua kununua magunia 11 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wanaosoma katika shule ya Msingi Bugoyi A na B pamoja na shule ya msingi Ndembezi ili mahindi yatumike kwa ajili ya uji wawapo shuleni huku magunia mengine yakigawiwa kwa wakazi wa kata hiyo.

Magunia hayo yakishushwa katika shule ya Bugoyi A.Pamoja na juhudi za kusaidia wanafunzi hao lakini magunia hayo yalionekana kuwa na dosari kutokana na magunia hayo kuwa na ujazo usiotakiwa.  Hiki ndicho alichosema Diwani huyo.....
“Lengo lilikuwa ni kutaka wanafunzi wetu wapate uji bila ubaguzi, lakini pia kuwahamasisha wazazi kuchangia suala la uji kwa watoto wao, nikawashirikisha wenyeviti wa vijiji wakakubaliana na wazo langu, ,nikanunua magunia 11 kwa pesa zangu,kila gunia likigharimu shilingi elfu tano lakini nashangaa kuona magunia haya yakiwa hayana ujazo unaotakiwa,yako pungufu”,alieleza Diwani huyo.
 “Katika shule hizi kuna baadhi ya wanafunzi hawana uwezo  wakulipia uji ,sikuwa  na nia mbaya,kwa ubunifu wangu nikaona mahindi haya ya msaada  mbali na kuwasaidia wanakijiji lakini pia yawasaidie  wanafunzi wetu ,kwa shule ya Bugoyi A,magunia matatu,Bugoyi B magunia matatu na Ndembezi magunia matano",aliongeza

Ni katika shule ya Msingi Bugoyi A baada ya mahindi kuwekwa kwenye mifuko huo ndiyo mwonekano halisi wa magunia hayo.Akizungumzia kuhusu dosari ya mahindi hayo,Afisa mtendaji wa kata ya Ndembezi James Dogani aliyekuwa anasimamia zoezi zima la kugawa mahindi katika kata hiyo alisema suala la upungufu wa mahindi katika magunia linatokana na wananchi kujichagulia magunia na kwamba kuna mahindi yalimwagika mwagika wakati wa zoezi la kugawa mahindi hayo.

Afisa kilimo wa manispaa ya Shinyanga Jeremiah Inegeja alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu dosari katikak magunia hayo ya mahindi alisema hakuna upungufu wowote na kwamba tumwulize afisa mtendaji wa kata pengine ndiyo anajua upungufu umetokana na nini.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugoyi B Anord Rweshabura alishukuru kupokea mahindi hayo na kuongeza kuwa hataruhusu mahindi hayo yatumike hadi pale yatakapoletwa mahindi mengine kujazia  magunia hayo kwani sasa hivi yako pungufu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post