MBUNGE wa Viti Maalumu, Mchungaji Getrude Rwakatare (CCM) wa
Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Mikocheni B, jijini Dar es
Salaam, ametengwa katika Ushirikiano wa Makanisa baada ya kanisa lake
kulalamikiwa kufungisha ndoa inayodaiwa kukiuka taratibu za kikanisa,
kisheria na kimaadili, Tanzania Daima Jumatano limejulishwa.
Ndoa inayolalamikiwa kufungishwa na kanisa hilo ni ile iliyoibuliwa
na gazeti hili wiki iliyopita ambayo inamhusisha Mbunge wa Viti
Maalumu, Rosweeter Kasikila (CCM) mwenye umri wa miaka 60 na kijana
Michael Christian wa miaka 26.
Ndoa hiyo ambayo ilifungwa katika kanisa hilo Septemba Mosi mwaka
2011, imebaki kuwa gumzo na kuwaacha hoi baadhi ya mawaziri, wabunge
pamoja na majirani wanaoishi jirani na mbunge huyo mjini Bagamoyo,
Pwani.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na
Haki za Jamii ya makanisa hayo, Mchungaji William Mwamalanga, alisema
uamuzi wa kulitenga kanisa la Mama Rwakatare umetokana na kikao cha
Kamati ya Maadili iliyokutana jana jijiji Dar es Salaam.
Alisema Kanisa la Mchungaji Rwakatare halifai kuendelea kuwa katika
ushirika huo kutokana na kubariki ndoa hiyo aliyodai kuwa ni batili.
Mchungaji Mwamalanga alisema utaratibu wa ndoa katika makanisa
unafahamika, ikiwa ni pamoja na wafungaji wa ndoa kutakiwa kutangaza
ndoa hiyo hadharani kwa kipindi cha wiki tatu.
“Ndoa hii haikutangazwa hadharani, kibaya zaidi inasemekana imefungwa
ndani ya ofisi na sio kanisani. Hiyo haiwezi kuitwaa ndoa maana
haijakidhi vigezo na taratibu za kikanisa, ni lazima Mchungaji Rwakatare
awajibike,” alisema.
Alisema lazima nyumba za ibada zikubali kutogeuzwa kichaka cha
kusaidia uovu kama ilivyofanywa na kanisa hilo la Mikocheni B kwa
kukubali kufanikisha ndoa hiyo kinyume cha taratibu.
“Tunalaani ndoa hiyo kuanzia mawio hadi machweo kwa kuwa hata
maandiko ya kitabu kitakatifu cha Biblia kinawathamini yatima kama
alivyo huyo kijana Michael anayeonekana kutoafiki ndoa hiyo kwa matakwa
yake,” alisema mchungaji huyo.
Alisisitiza kuwa wanamtenga Mchungaji Rwakatare na kanisa lake kwani
amewachafua na kuyatia aibu makanisa mengine yote nchini.
Mchungaji huyo pia alimtaka Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya
Kikwete kuwaengua kwenye chama hicho Mchungaji Rwakatare na Kasikila
kuhusiana na ndoa hiyo.
“Rwakatare ni mtunga sheria, anajua wazi kuwa ndoa inatakiwa pia
kubandikwa katika ubao wa matangazo. Ni wazi kuwa wameamua kuvunja
sheria na kutenda kosa la jinai,” alidai.
Mwamalanga alisema kuwa kwa hatua hiyo ndoa hiyo ni batili na haramu
kwa kuwa ni aibu pia kwa mtoto kumuoa mwanamke mwenye umri wa mama
yake.
Katika hatua nyingine, mchungaji huyo alisema umoja wao unafanya kila
iwezalo kuhakikisha kijana Michael anarudishiwa vyeti vyake ambavyo
kwa sasa vimezuiliwa na Mbunge Kasikila.
Pia aliitaka Kamati ya Maadili ya Bunge kuwaita na kuwahoji wabunge
hao kwa kitendo chao cha kuhalalisha ndoa hiyo kwani kimeutia doa
muhimili huo.
Alisema Bunge ni sehemu tukufu, hivyo Rwakatare na Kasikila hawana hadhi ya kukaa huko, hivyo alishauri waenguliwe.
Alipopigiwa simu kueleza msimamo wake juu ya uamuzi wa umoja wa
makanisa hayo kumtenga kwa kuhalalisha ndoa hiyo, Mchungaji Rwakatare
aling’aka na kukata simu.
Alipopigiwa tena simu yake ilizimwa na hakuweza kupatikana tena hadi tunaenda mitamboni.