MAJI YAVUNJA NDOA KATIKA WILAYA YA KISHAPU,MKOANI SHINYANGA



Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano kutoka TGNP Bi Lilian Liundi akizungumzia mafanikio ya TGNP tangu ianzishwe mwaka 1993  katika warsha ya siku tatu kwa waandishi wa habari kuhusu harakati za mwanamke na mchakato wa katiba mpya iliyoandaliwa na Mtandao wa jinsia Tanzania TGNP

Imeelezwa kuwa wanawake wengi katika wilaya ya kishapu iliyopo mkoani shinyanga wanakabiliwa changamoto ya kuvunja ndoa zao kutokana na umbali uliopo ili kupata huduma ya maji,ambapo hulazimika kuamka kila siku saa 11 alfajiri kufuata hduma ya maji kwa  takribani kilomita kumi na tayari ndoa zaidi ya kumi zimevunjika kwa sababu hiyo.


Hayo yamebaishwa leo na wananchi wa wilaya hiyo   katika warsha ya siku tatu inayoendelea, kwa waandishi wa habari kuhusu harakati za mwanamke na mchakato wa katiba mpya iliyoandaliwa na Mtandao wa jinsia Tanzania TGNP katika viwanja vya Mazingira Senta mjini Shinyanga.


Mmoja wa washiriki katika warsha hiyo Bi Sesilia John,kutoka Kikundi cha Nyuki cha Kishapu ambacho kiko chini ya TGNP amesema  wanawake wengi wa Kishapu wanavunja miji yao  kutokana na adha ya maji ambapo hulazimika kuwaacha wanaumme wao kila siku saa 11 alfajiri  hali inayosababisha wanaumme hao kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake wengine,matokeo yake ndoa zinavunjika.


“Wanawake wa kishapu pia wanabakwa,kupigwa na hata kuvamiwa na wanyama aina ya fisi pindi wanapofuata huduma ya maji nyakati za usiku,mfano katika kijiji cha Lubaga na Isoso,na ukosegu huu wa maji pia unasababisha hata kufa kwa mifugo yetu”,Bi Sesilia amesema.

 Naye mwenyekiti wa Kikundi hicho cha Nyuki Bi Anna Christopher amesema licha ya kuwepo kwa tatizo la maji pia shule nyingi za sekondari wilayani humo hazina walimu wa kutosha,michango katika shule pia ni mingi sana, na jambo la kushangaza shule ya  sekondari Isoso iliyojengwa mwaka 2006 haina hata mwanafunzi mmoja.

Katika hatua nyingine Afisa wa Habari na mawasiliano wa TGNP,Bi Scholastica Makwaia,amesema hivi karibuni mtandao wa jinsia Tanzania ulifanya ziara ya wiki tatu wilayani humo na kubaini kuwa bado kuna ukatili kwa wanawake,na aliainisha aina mbili za ukatili huo yaani ukatili wa kimwili na ule wa kiuchumi ambapo mwanamke hutumia muda mwingi kulima na wakati wa mavuno wanaumme ndio wanakuwa wauzaji wakuu wa mazao yaliyopatikana.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano kutoka TGNP Bi Lilian Liundi ametaja miongoni mwa malengo ya warsha hiyo kuwa ni kuendelea kujenga uelewa kwa wanahabari kuhusu harakati za ukombozi wa wanawake kwenye mchakato wa uundwaji wa katiba mpya.

Amefafanua pia kuwa warsha hiyo ni kutafakati kwa pamoja miaka 20  ya harakati za wanawake TGNP ambayo ilianzishwa mwaka 1993,pamoja na tamasha la jinsia mwaka 2013, sambambamba na kujadili mikakati ya baadae katika kupashana habari kuhusu mambo ya jinsia katika jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

1/Post a Comment/Comments

  1. hizo nyingine ni chai tu. nani kasema michango mingi? mlalamikaji afike idara husika apewe maelekezo

    ReplyDelete

Post a Comment