*TAMKO - STATEMENT YA ASKOFU METHOD KILAINI DHIDI YA GAZETI LA MWANANCHI LEO NOVEMBA 16 2012Askofu Method Kilaini

TAMKO – STATEMENT

Kwa masikitiko makubwa nimesoma katika gazeti la Mwananchi kwamba nimeiponda safu ya uongozi na sekretariati ya CCM. 
 
Mimi sijaongea na gazeti lolote juu ya uongozi wa CCM na wala sina nia au sababu ya kuuponda uongozi huo.  
Ni vibaya kwa gazeti lo lote lile kutumia jina la mtu kwa kueneza maoni yake. Kama ni waugwana natumaini watasahihisha waliyoyaandika. 
 
 Nasikitika sana kwa walikwazwa na hilo. Askofu Kilaini

Askofu Method Kilaini
       Bukoba Catholic Diocese
  Source:kagerayetu

    HABARI KUTOKA GAZETI LA MWANANCHI ILIYOLETA SHIDA HII HAPA

Sekretarieti mpya CCM yapondwa kila kona

KILAINI, WASOMI WASEMA HAKUTAKUWA NA JIPYA,DK SLAA ADAI IMEJAA WATUHUMIWA WA UFISADI

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kutangaza safu mpya ya wajumbe wa Sekretarieti ya chama hicho, wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini wameponda uteuzi huo wakisema chama hicho tawala, kisitarajie jipya kutoka katika safu hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, wadau hao walisema viongozi  walioteuliwa wana upungufu, hivyo hawawezi kuwajibishana kwa kuwa wanaogopa kuumbuana.

Katika uteuzi huo Kikwete aliwateua, Abdulrahaman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM, akisaidiwa na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba upande wa Bara na Vuai Ali Vuai upande wa Zanzibar.

Wengine ni Zakhia Meghji aliyeteuliwa kuwa Katibu wa Uchumi na Fedha, Mohamed Seif Khatib (Oganaizesheni), Dk Rose Migiro (Kimataifa) na Nape Nnauye (Uenezi).

Uteuzi huo ulitanguliwa na uchaguzi ambao ulimrejesha Kikwete kuwa Mwenyekiti wa chama wa Taifa akisaidiwa na Philip Mangula (Tanzania Bara) na Dk Ali Mohamed Shein (Zanzibar).

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanawatizama Mangula na Kinana kama viongozi makini, lakini wasioweza kumudu kasi ya siasa za sasa ambazo zimebadilika kulingana na wakati na aina ya ushindani kutoka upinzani.

Kadhalika wanakiona kikosi hicho kuwa hakiwezi kuisaidia CCM kupambana na rushwa, ambayo inaonekana kuota mizizi kiasi cha kuonekana kama sehemu ya utamaduni wa chama hicho.

Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Methodius  Kilaini alisema safu hiyo ya uongozi haina jipya akifafanua kuwa, tatizo kubwa la chama hicho ni mfumo wake wa utendaji kazi.

“Ni mfumo ambao wamejiwekea wa kulindana, hivyo uongozi huu hautaleta mabadiliko yoyote    CCM,” alisema Kilaini.

Alisema viongozi waliochaguliwa hawatakuwa na sauti  kwa kuwa nao wana udhaifu wao hivyo hawawezi kuwachukulia hatua wenzao kwa kuwa nao wataumbuliwa.

Askofu Kilaini alisema  viongozi hao wataendeleza mfumo walioukuta na hakuna atakayeweza kumkosoa mwenzake aliyefanya makosa.

“Kati ya viongozi wa CCM waliochaguliwa hakuna atakayemnyooshea mwenzake kidole kwamba amefanya kosa fulani, ni vigumu mno kumwadhibu mwenzake kwa kuhofia kuwa, kwa vile yeye pia ni dhaifu akimwadhibu huyo matendo yake yatagundulika,” alisema.

Alisema licha ya Rais Kikwete kukemea rushwa kwa viongozi wote waliochaguliwa, lakini hakuna hatua yeyote aliyochukuwa kwa wale waliotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo wakati wa chaguzi za ndani ya CCM.

“Rais wetu anazungumzia rushwa  na kukemea lakini  hakuna aliyemchukulia hatua yoyote kwa wale waliokutwa wakitoa rushwa  katika uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Jumuiya ya Wazazi na Ujumbe wa Halmashauri Kuu (Nec),” alisema Kilaini.
Kauli za wasomi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema Watanzania wasitegemee mabadiliko katika safu mpya ya uongozi ya CCM kwa kuwa walioteuliwa hawana jipya.

“Mangula ni kiongozi mwenye sifa nzuri kutokana na kusimamia misingi ya TANU ndani ya CCM, ila msimamo wake hauwezi kufanikiwa katika kipindi hiki kwa sababu sura ya chama ni tofauti na mtizamo alionao,” alisema Dk Mkumbo.

Alisema Kinana licha ya kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM tangu utawala wa Serikali ya awamu ya tatu, lakini hakuweza kuleta mabadiliko yoyote ndani ya chama hicho.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idris Kikula alisema utendaji kazi wa viongozi hao wapya hauwezi kutabiriwa kwa sasa, kwani ni mapema mno.

Alisema kuwa, viongozi hao wanatakiwa kupewa muda wa kufanya kazi zao na kwamba kuwasema kwa sasa ni sawa na kuwahukumu bila kosa lao.

Profesa Kikula alisema kuwa, aliufuatilia kwa makini uchaguzi huo na kubaini kuwa jambo lililotakiwa kufanyiwa kazi zaidi ni tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya makada wa chama hicho.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk George Shumbusho alisema licha ya baadhi ya viongozi hao kuwa na sifa nzuri, changamoto inayowakabili ni kutokomeza rushwa ndani ya chama hicho tawala.

“Mangula na Kinana ni viongozi wazuri, ila hawawezi kuleta mabadiliko bila ya kupata ushirikiano kutoka kwa wanachama wengine, mzigo mkubwa walionao ni kuhakikisha kwamba wanaondoa tatizo la rushwa,” alisema Shumbuso.

Shumbusho alisema kuwa kama CCM haitachukua uamuzi mgumu kwa wanachama wake bila kujali urafiki, haitaweza  kumaliza tatizo la rushwa na itaendelea kupigiwa kelele na wapinzani na wananchi.

Ofisa Elimu Mwandamizi wa chuo kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Simon Shayo yeye alisema: “Sidhani kama kuna mabadiliko yatakayojitokeza ndani ya CCM kwa sababu viongozi ni walewale, changamoto ndani ya chama hiki haziwezi kuondolewa na wazee hata kama baadhi yao wanaonekana kuwa na sifa.”

Shayo alisema kipindi hiki kilikuwa ni nafasi ya vijana kupewa nafasi ya kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho kwa sababu ndiyo wenye nia ya dhati ya kukiletea mabadiliko.
Wanasiasa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kuwa  safu hiyo mpya haiwezi kupambana na ufisadi na kutekeleza dhana ya kujivua gamba kwani wengi ni watuhumiwa wa ufisadi.

Alitoa mfano wa kashfa ya wizi wa mabilioni ya Fedha za Akaunti ya Nje (EPA) kutoka Benki Kuu (BoT) na utoroshaji wa nyara na fedha za umma nje ya nchi, alisema uteuzi huo umelenga kufukia  madhambi ya ufisadi unaowakabili viongozi wengi kwenye chama hicho na serikalini.

Katika maelezo yake Dk Slaa ukiwachunguza viongozi hao mmojammoja utabaini kwamba kila mmoja ana matatizo yake ya kutuhumiwa katika jambo moja au jingine na kwamba katika mazingira ya aina hiyo, hakuna matumaini ya kuwapo kwa mabadiliko.

“Ni kwa sababu tu watu wanasahau, naona watu wanasema hiyo ni safu mpya, wengine wanasema safu ya ushindi, mimi nasema hakuna upya wowote hapo, wala hakuna safu ya ushindi,” alisema Dk Slaa na kuongeza;

“Safu hiyo imeundwa ili kuendelea kulinda ufisadi ambao umeendelea kukididimiza chama hicho na Serikali yake,  lengo ni kufukia na kupanga mikakati ya kufanikisha ufisadi mwingine kwa ajili ya kuendelea kuwa madarakani kwa CCM.”

Alisema kuwa ili Watanzania waweze kupiga hatua, taifa linatakiwa kuwa na viongozi ambao hawahusishwi na kashfa za ufisadi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema hakuna jipya katika sekretarieti  hiyo mpya licha ya kuwarudisha wakongwe.

“Nilitegemea vijana wangepewa nafasi kubwa katika uteuzi huo kwa kuwa hivi sasa vijana ndiyo chachu ya ushindi katika kila chama, halafu wakongwe wakabaki  washauri, lakini imekuwa sivyo,” alisema Ruhuza.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julias Mtatiro alisema kuwa, watu ni walewale walioteuliwa kushika nafasi hizo hivyo hakuna mabadiliko yoyote yatakayokea.

“Sidhani kama uteuzi huo utasaidia kuleta maendeleo katika chama chao na hata katika taifa kwa sababu ndicho chama tawala,” alisema Mtatiro na kuongeza;

“Wote walioteuliwa walishawahi kushika nafasi za juu katika Serikali kupitia chama hicho, hivyo hakuna jipya walilofanya”.

Imeandaliwa na Bakari Kiango, Fidelis Butahe, Kelvin Matandiko, Peter Elias, Magreth Munisi na Pamela Chilongola.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments