Baada ya Kutishiana: Tanzania, Malawi wakutana Dar Kuzungumza

Mkutano kati ya Tanzania na Malawi kujadili suluhu ya mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa umeanza katika ngazi ya Wataalamu jijini Dar es Salaam tarehe 15 Novemba, 2012.

 Mkutano huo unaowahusisha wataalam kutoka Wizara na Idara mbalimbali za Serikali za Tanzania na Malawi unafanyika Jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Tanzania akiwemo Mhe. Balozi Patrick Tsere (wa pili kutoka kushoto), Balozi wa Tanzania nchini Malawi na Balozi Irene Kasyanju (kushoto) wakimsikiliza Bw. Chisi (hayupo pichani) wakati wa mazungumzo hayo.

 Akifungua Mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule alisisitiza umuhimu wa wajumbe kutoka nchi zote mbili kujadili na kupendekeza njia zitakazosaidia kupata suluhisho la kudumu la mgogoro huo.

 Aidha, Bw. Haule aliweka bayana kuwa Serikali ya Tanzania ina dhamira ya dhati kufanya kazi pamoja na Serikali ya Malawi kutafuta suluhu ya mgogoro huo jambo ambalo pia lilisisitizwa na Bw. Julius Chisi, Kiongozi wa Ujumbe wa Malawi.

 Mkutano huo ambao utafanyika kwa siku tatu hadi tarehe 17 Novemba, 2012 umeanza na Kikao cha Wataalamu ambacho kitafuatiwa na kikao cha Maafisa Waandamizi na kuhitimishwa na kikao cha Mawaziri tarehe 17 Novemba, 2012.
Bw. Julius Chisi, Naibu Mpimaji Ardhi Mkuu kutoka Malawi  akizungumza machache wakati wa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. John M. Haule, akifungua Mkutano wa Timu ya Pamoja ya Wataalam kati ya Tanzania na Malawi kuhusu mgogoro wa mpaka kwenye Ziwa Nyasa. Mkutano huo uliowahusisha wataalam kutoka Wizara na Idara mbalimbali za Serikali za Tanzania na Malawi unafanyika  Jijini Dar es Salaam katika Hoteli ya Serena.
(Picha na Habari kwa hisani ya Blog ya Michuzi)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post