SAKATA LA MGOGORO WA MPAKA NDANI YA ZIWA NYASA KATI YA TANZANIA NA MALAWI LACHUKUA SURA MPYA. -Wazee Kyela watoboa siri nzito.
WAKATI nchi ya Malawi ikiendelea kushikilia msimamo wake, kuwa halali ya mpaka Mashariki mwa ziwa Nyasa kati yake na Tanzania unatenganishwa na ardhi ya Tanzania, Wazee wilayani Kyela, wametoboa siri na kuweka hadharani ukweli wake.
Wazee wengi waliotoa ushahidi juu ya ukweli wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ndani ya ziwa nyasa, mbele ya msafara wa ziara ya siku moja ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe ni wale waishio kando kando ya ziwa hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mstaafu, John Mwakipesile (70), ambaye katika maelezo yake akiwa wa kwanza, alisema anashangazwa na madai hayo mapya ya Malawi kuwa Ziwa lote ni miliki yao.
Alisema kitendo hicho cha nchi hiyo kukurupuka kinapaswa kuupuzwa kwa kuwa jambo hilo halina ukweli na linapingana na historia na desturi za kweli za maisha ya kawaida ya wananchi wa mpakani wa mataifa haya toka enzi za ukoloni.
Alisema madai ya Malawi hayajazingatia historia ya kweli ya ziwa hilo kwani madai yao yote ni kujaribu kuficha ukweli kwa kuwa yeye kama kizazi cha tatu hata siku moja hakuwahi kusikia kuwa ziwa lote ni mali ya nchi hiyo.
Alisema kuna ushahidi wa kutosha juu ya Tanzania kuwa miongoni mwa wamiliki wa ziwa hilo, kwani kuna mali za watanzania ikiwemo Makaburi yamepotelea ndani ya ziwa hilo baada ya kumezwa.
Alitolea mfano shule ya Msingi aliyesoma katika mwaka 1945 kuwa ilishamezwa na ziwa hilo, yakiwemo majengo ya baraza (Mahakama) katika kijiji alichozaliwa cha Mwaya katika wilayani humo.
“Mimi kwa umri wangu wa miaka 70 ni kizazi cha tatu katika Wilaya hii nakumbuka shule niliyosoma mwaka 1945 pale Mwaya nilipozaliwa ilishamezwa na Ziwa na ni umbali wa kilomita mbili toka pwani ya sasa kijijini hapo” alifafanua Mwakipesile.
Naye Maini Mwakisambwe(83), Mkazi wa kata ya Katumba songwe, alisema tangu azaliwa alikuwa akijua mpaka ni Mto Songwe ambao unaingiza maji ndani ya ziwa hilo na ndio uliotumika kama mpaka wa kuligawa ziwa klwa mataifa haya mawili.
Mbali na hilo, lakini pia wakiwa vijana walishuhudia viongozi wa serikali zote mbili wakiheshimu mpaka huo ndani ya ziwa , kwa kuwa hata waliposafiri toka upande mmoja kwenda mwingine kila wakifika eneo la Mto Songwe bendera ya uapane mmoja ilishushwa na kupandishwa ya upande mwingine.
Philipo Mwandemele(73) kabla ya kuanza kutoa maelezo yake alitoa kitabu kimoja kinachozungumzia maisha na desturi za wakazi wan chi hizi mbili kama nyaraka muhimu inayoweza kutumika kueleza ukweli juu ya sakata hilo la mpaka.
Katika kitabu hicho kilichoandikwa na mmishenari kutoka nchini Ujerumani Teodoro Mayers , anayedaiwa kufika wilayani humo kwa lengo la kueneza dini , katika ukurasa wake wa 31 kinathibitisha kuwa mwaka 1891 kulikuwa na mapatano kati ya Ujeruman na Uingereza kuwa mpaka wa Tanzania na Malawi ndani ya ziwa unaanzia pale Mto Songwe unamwaga maji ndani ya ziwa hilo.
Kutokana umuhimu wa kitabu hicho chenye jina la Wakonde, mila na Desturi za Wanyakyusa, Waziri wa Mambo ya Nje Membe alimuomba kuiazima serikali kwa muda ili kikarudufiwe na baadae kurejeshewa kwa lengo la kupata ushahidi sahihi.
Waziri Membe akihitimisha ziara hiyo alisema licha ya nchi ya Malawi kuonekana kusuasua katika vikao, kamwe Tanzania haitarudi nyuma kushughulikia mgogoro huo na kwamba hadi kufikia mwaka 2015 suala hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi.
Aliongeza kuwa maelezo na ushahidi huo uliokusanywa kwa wakazi wa wilaya ya Kyela utatumiwa na serikali katika Mahakama ya kimataifa ya Usuluhishi ya (ICJ), kama suluhu ya mashauriano ya pande mbili yatashindikana.
Katika mazungumzo juu ya mgogoro wa mpaka katika ziwa Nyasa yaliyofanyika Agosti mwaka huu nchini Malawi, Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa kimataifa wan chi hiyo Epraim Chiume, akihitimisha maelezo yake alisisitiza kuwa licha mgogoro huo kuhitaji busara zaidi , serikali yake inaamini kuwa mpaka kati ya nchi hizo upande wa mashariki mwa ziwa Nyasa unatenganishwa na ardhi ya Tanzania.

Kwahisani ya Moshi Mathias,Kyela.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post