MGANGA WA FREEMASON AJITOKEZA IRINGA


Ukisoma mabango haya niliyokuwekea kwenye ukurasa huu leo, hutapata shida kutambua kuwa matatizo mengi ya Watanzania, si tu kwamba yanasababishwa na wanasiasa.
Ndiyo maana nimejiepusha kujadili Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na uteuzi wa viongozi wapya wa Sekretarieti ya chama hicho. Kwa ufupi ni kwamba matatizo ya Tanzania na Watanzania ni zaidi ya siasa na wanasiasa.
Ukisoma ujumbe ulio kwenye mabango haya unauona upumbavu unavyotamalaki katika jamii yetu. Bahati nzuri kwa wanaosambaza upumbavu huo ni kwamba wapo wanaouamini, na kwa sabahu hiyo wamewafanya matapeli hawa waendelee kuwapo na wengine wazidi kuibuka kila uchao.
Kwanza, nisema kwamba tatizo la imani za kishirikina na ujinga wa kuamini ndumba vimeenea sehemu nyingi duniani. Masuala hayo yapo pia Ulaya, Marekani na Asia. Tofauti iliyopo ni viwango na aina za uongo; pamoja na idadi ya watu walio wafuasi wa mambo hayo.
Hapa kwetu hali ni mbaya. Mauaji ya albino ni aina ya ujinga huo. Dunia ya leo bado kuna watu wanaamini kuwa kiungo cha albino kinaweza kuwatajirisha.
Pamoja na ukweli kwamba Katiba yetu imewapa wananchi uhuru wa kuabudu (kuamini?), kuna mambo tunayopaswa kuyahoji. Upuuzi huu unafanywa mbele ya Serikali ilhali ikitambua kuwa wanaoendesha mambo haya ni waongo, matapeli, majizi na watu waliodhamiria kuviza akili na maendeleo ya Watanzania.
Wapuuzi hawa walianza kujitangaza kwa majina na mahali wanakoishi. Maendeleo ya teknolojia yamewawezesha kumiliki simu. Matangazo yao yanapambwa kwenye kila kona hapa nchini. Haitashangaza kuyaona kwenye ukuta wa Ikulu!
Walianza kudanganya kuwa wanatibu Ukimwi. Serikali haikuchukua hatua madhubuti kukanusha upuuzi huo. Wananchi wenyewe hawakuamini kuwa huo ni uongo. Hatua hiyo haijawakatisha tamaa, maana wateja wapo japo ni wachache.
Sasa wameibuka na mambo mengine hatari. Wapo wanaojitangaza kwamba wana uwezo wa dawa wa kumfanya mwanafunzi afaulu mitihani! Wamelenga kuwapata wanafunzi wa shule za msingi, vyuo na sekondari.
Kwa maneno mengine ni kwamba mwanafunzi asisome kwa bidii. Atulie tu, siku ya mtihani atashinda kwa sababu dawa ya kumwezesha kushinda imeshapatikana! Ujinga huu unapatikana Tanzania, na pengine Afrika pekee!
Wameibuka wengine wanaeneza ujinga kwamba wana uwezo wa kumfanya mtu apandishwe cheo kazini! Huu ni upumbavu wa hali ya juu. Kama kweli dawa hizo zipo, basi jeshini wote wangekuwa majenerali! Kusingekuwapo koplo wala sajini!
Kama kweli kuna dawa ya vyeo, basi nchi hii kila mtu angekuwa mkurugenzi, au waziri, au katibu mkuu, au rais! Badala ya watu kufanya kazi kwa weledi na juhudi, wanaaminishwa kwamba dawa zitawawezesha kupata vyeo vya juu! Ujinga mtupu.
Wapo wanaojitanabaisha kuwa na dawa za kurejesha mali zilizoibwa. Huu nao ni uongo tu. Kama hivyo ndivyo, kwanini hawajajitokeza kumsaidia Zitto Kabwe ili mabilioni yaliyofichwa ughaibuni yarejeshwe? Kwanini Serikali itumie gharama kubwa kuendesha kesi za ufisadi ilhali kuna “wataalamu” inaoweza kuwatumia kurejesha fedha hizo?
Wapuuzi hawa wanajigamba kutibu kisukari, wakati wanatambua kuwa hakuna dawa ya kutibu maradhi hayo. Kama ipo, wanasubiri nini kuisambaza duniani ambako matajiri wengi wanasumbuliwa na maradhi hayo?
Wengine wanasema wana dawa za mapenzi kiasi kwamba kama mwanamme akimtaka mwanamke, atampata! Au mwanamke akimtaka mwanamme, atampata! Huu ni uongo mwingine. Kuna binti gani wa Kitanzania asiyependa kuolewa katika ukoo wa kifalme?
Mbona hatujasikia kina Prince Charles kutoka ughaibuni wakifika hapa nchini kwa mvuto wa dawa hizo kuleta posa kwa mabinti zetu? Mbona hatujasikia kijana mvulana wa Kitanzania kaenda kuoa katika ukoo wa mfalme Hirohito au Akihito huko Japan?
Tunahangaika na dawa za kuongeza nguvu za kiume, dawa za kufauli mitihani, dawa za mvuto wa biashara na ujinga mwingi; huku tukiwaacha wazungu, wahindi na waarabu wakijitwalia malefu ya ekari za ardhi yetu.
Tufanye nini? Upuuzi huu lazima tuhakikishe unakomeshwa katika jamii yetu. Kazi ya kuukomesha imerahisishwa na matapeli hao wenyewe kwa kuweka namba za simu kwenye mabango yao. Serikali za Mitaa hazipaswi kufumbia macho ujinga huu.
Matangazo haya yanaifanya jamii ya Watanzania ikose weledi wa kupambana na maisha kwa njia za kisayansi. Yanawafanya wananchi wengi waamini kuwa unaweza kusafishwa nyota kisha ukaamka ukiwa tajiri! Hizi ni athari za kupenda njia za mkato. Watanzania tunapenda sana mkato.
Matangazo haya ni wizi wa fedha kutoka kwa watu wenye uelewa mdogo, na hasa kutokana na uhaba wa elimu na umasikini. Matangazo haya yanakifanya kizazi chetu kiwe cha mbumbumbu wanaoamini katika mitishamba, miujiza, ngekewa; na si katika kujisomea au kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Imani hizi zinatufanya tusiwe na utashi wa kujenga mabweni, maabara wala nyumba za walimu au hata kuweka madawati katika shule zetu! Hatufanyi kazi hizo kwa sababu tumeaminishwa na wapuuzi hawa kwamba hata bila maabara, vitabu, vyumba bora vya madarasa, nyumba za walimu na walimu waliohitimu vizuri, bado tutashinda mitihani na mwisho tutayashinda maisha!
Matapeli hawa wanawaumiza wananchi kiuchumi. Serikali nayo imebariki wananchi wake waumizwe. Fedha ambazo wananchi wanahangaika kuzipata, wanazipeleka kwa watu hawa kwa matarajio ya kufanikiwa zaidi. Huu ni wizi. Matapeli hawa wanapaswa kushitakiwa kwa makosa ya wizi na ulaghai.
Haya niliyoyasema kwa matapeli hawa wa mitaani, nayasema pia kwa matapeli wa makanisani. Huko nako tunaaminishwa kuwa kusali pekee kunaweza kubadili maisha yetu. Tunadanganywa. Kumeanzishwa redio eti za kuendesha maombi kwa sadaka zinazopelekwa kwa njia ya Tigo-Pesa, M-Pesa, na kadhalika. Wizi tu.
Jamii iungane kutokomeza imani hizi za kipuuzi. Tufanye hivyo kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.
source;rizikimgaya blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post