WALIMU WATOBOA MAHUSIANO YA MWENZAO, RPC BARLOWBaadhi ya walimu wa Shule ya Msingi Nyamagana wamevunja ukimya na kueleza kile kinachodaiwa ni mahusiano kati ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Leberatus Barlow, na mwalimu mwenzao, Dororth Moses.

Wakizungumza na NIPASHE shuleni hapo jana, pia walielezea kusikitishwa kwao na jinsi tukio hilo la mauaji ya RPC lilivyotokea mbele ya mwalimu mwenzao, Doroth Moses aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi eneo la Kitangiri, jijini Mwanza.

Mwalimu Doroth ndiye aliyekuwa na RPC Barlow ndani ya gari wakati watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walipowavamia na kumuua kwa kumpiga risasi Kamanda huyo.

Katika mahojiano hayo Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Mary Ngalula, alisema wanamuonea huruma mwalimu mwenzao kutokana na kushuhudia tukio hilo la kutisha.

Alisema wanamsikitikia kwa sababu jamii imeanza kumfikiria vibaya kwa kudhani anahusika kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo.

“Tunamuonea huruma mwalimu mwenzetu kutokana na maneno tunayoyasikia, lakini sisi tuko pamoja naye kwa sababu tunamfahamu ni mtu safi, na hivi tunajiandaa kwenda kumuona na kumtia moyo ili amudu kuilea familia yake kwani ni mjane,” alisema.

Mwalimu Baraka Magafu alisema tofauti na hisia za baadhi ya watu kuhusu uhusiano wa Mwalimu Doroth na Kamanda Barlow, wao (walimu) wanafahamu kuwa ni watu wa kabila moja wanaotoka kijiji kimoja huko Vunjo mkoani Kilimanjaro.

Alibainisha kuwa Mwalimu Doroth amekuwa ni mtu anayejihusisha sana na shughuli mbalimbali za watu wa kabila lake (Wachaga), hivyo hakuna sababu ya kumfikiria vibaya kwa sababu tu mtu aliyekuwa amemsindikiza nyumbani wakitokea kwenye kikao cha maandalizi ya harusi aliuawa kwa kupigwa risasi.

“Ukifuatilia mwenendo wa tukio lote, utaona kwamba kilichotokea ni bahati mbaya na kingeweza kumtokea yeyote, kwani Barlow alikuwa akimsindikiza Mwalimu Doroth nyumbani kwake, na hata baada ya tukio, alipowapigia simu wenzao waliokuwa nao kwenye kikao walikuwa ndipo na wao wanafika majumbani mwao,” alisema.

Aliongeza kwamba katika mazingira kama hayo ni makosa kuwa na mtazamo hasi dhidi ya Mwalimu Doroth kama ambavyo baadhi ya watu wameanza kuvumisha kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Wakati huo huo, majonzi, simanzi na kauli za kulipa kisasi ni miongoni mwa mambo yaliyogubika shughuli ya kuuaga mwili wa  Barlow.

Mwili wa Barlow uliagwa na wakazi wa Jiji la Mwanza wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, katika shughuli iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana jana.

Baada ya shughuli ya kuagwa mwili wa Barlow, ulisafirishwa baadaye jana jioni kwa ndege kuelekea jijini Dar es Salaam kabla ya leo kusafirishwa kwenda kijijini kwake Vunjo, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
Chanzo:nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments