ANZISHENI HIFADHI ZA VIJIJI KUPITIA MRADI WA LTIP - PINDA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akizungumza katika Mkutano wa wadau kuhusu Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika halmashauri ya Kilwa mkoani Lindi baada ya kuufungua tarehe 23 Mchi 2024.

****************

Na Munir Shemweta, KILWA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amevitaka vijiji vilivyopangiwa mipango ya Matumizi ya Ardhi kupitia mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) kuutumia mradi huo kuanzisha hifadhi za vijiji ili kutunza na kuhifadhi misitu.

Mhe, Pinda ametoa kauli hiyo tarehe 23 Machi 2024 wakati akifungua mkutano wa wadau kuhusu Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi uliofanyika kiwilaya kwenye halmashauri ya wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi.

‘’Namna nzuri ya kutunza mazingira kwenye maeneo yetu ni kuanzisha miradi inayoweza kusaidia kutunza mazingira na misitu kwa kuanzisha WMA katika vijiji vyenu’’ amesema Mhe, Pinda

Amesema, vijana wanaweza kutumia hifadhi hizo za misitu zilizobainishwa na mradi wa uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi kwa kuanzisha miradi kama vile ufugaji nyuki ambapo amesema mradi huo unaweza kuwapa faida kubwa kiuchumi.

‘’Misitu yote iliyotengwa kupitia mradi wa LTIP makundi ya vijana yahamasishwe ili yaweze kufuga nyuki sisi kule kwetu tunafuga nyuki na lita moja ya asali tuko mbali kweli kweli’’ amesema Mhe, Pinda

Mmoja wa waratibu wa mradi wa LTIP wilaya ya Kilwa ambaye ni Afisa Mipango wa Miji wa Wizara ya Ardhi Elisha Mengele alieleza kuwa, mradi wa uboreshaji usalama wa Milki za Ardhi mbali na mambo mengine umelenga kuwa na maeneo ya hifadhi endelevu, kuondoa migogoro ya mipaka na uwezeshaji vyeti vya ardhi vya vijiji ili kuwa na nguvu ya kisheria kusimamia ardhi yao.

Amesema, kupitia mipango ya Matumizi ya ardhi kwenye halmashauri wilaya ya Kilwa maeneo mbalimbali yametengwa kama vile kupanga maeneo yatakayoendana na uhalisia sambamba na kuhakikisha misitu na maeneo muhimu kuhifadhiwa yanakuwepo.

Kwa upande wao, wananchi wa Kilwa wameonesha kuridhishwa na mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini kwa kuwa umewashirikisha na kutenga maeneo mbalimbali kama vile mifugo, wakulima, misitu ya asili, vyanzo vya maji pamoja na makaburi.

Wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji mradi huo walioueleza kuwa umempa haki kila mtu alipo.

‘’Mradhi huu utatupelela mbele zaidi kwa sababu kila mtu atajua hiki changu hiki cha mwenzangu na utatupeleka migogoro itaisha’’ walisema

Wizara ya Ardhi kupitia mradi wa LTIP awali ulichagua wilaya 7 za kutekeleza mradi ambazo ni Maswa, Mufindi, Tanganyika, Mbinga, Chamwoni, Longido na Songwe uliolenga kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kupanga ardhi katika vijiji 250, kupima na kusajili hati za Hakimiliki za kimila 500,000.

Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa wilaya 15 zilizoongezwa kunufaika na mradi wa LTIP kwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 69kati ya vijiji 90 vilivyopo katika halmashauri ya wilaya ya kilwa na kufanya vijiji vilivyofikiwa na mradi huo kuwa 1667 nchi nzima,
 Sehemu ya washiriki wa mkutano wa wadau kuhusu Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika ngazi ya wilaya uliofanyika wilayani Kilwa mkoa wa Lindi tarehe 23 Mchi 2024.
Afisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Elisha Mengele akielezea Mipango ya Matumizi ya Ardhi iliyotekelezwa wilayani Kilwa wakati wa mkutano wa wadau kuhusu Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi tarehe 23 Machi 2024.
Wataalamu wanaoshiriki katika Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda akisalimiana na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini Selemani Bungara maarufu kama ‘Bwege’ alipokwenda kufungua Mkutano wa wadau kuhusu Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika halmashauri ya Kilwa mkoani Lindi tarehe 23 Mchi 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post