
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwasili mkoani Shinyanga kesho Jumapili, Novemba 8, 2026, kwa ziara ya kikazi ya siku nne itakayohusisha wilaya na halmashauri mbalimbali za mkoa huo.
Akizungumza kuhusu ratiba ya ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema Dkt. Nchemba ataanza shughuli zake katika Wilaya ya Kishapu kwa kuhutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa SHIRECU.
Amesema Jumatatu, Novemba 9, Waziri Mkuu atatembelea Jimbo la Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambako atahutubia wananchi katika Uwanja wa Iselamagazi, kabla ya kuelekea Manispaa ya Shinyanga na kufanya mkutano mwingine wa hadhara katika Uwanja wa JASCO, Kata ya Ngokolo.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Jumanne, Novemba 10, Dkt. Nchemba atakuwa katika Jimbo la Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ambako atazungumza na wananchi katika Uwanja wa Usanda, Kata ya Usanda, kabla ya kuelekea Manispaa ya Kahama kwa mkutano wa hadhara utakaofanyika Kata ya Majengo.
Novemba 11, siku ya mwisho ya ziara yake, Waziri Mkuu atatembelea Halmashauri ya Ushetu na kuhutubia wananchi katika Uwanja wa Nyamilangano, Kata ya Nyamilangano, kisha kuelekea Halmashauri ya Msalala ambako atafanya mkutano mwingine wa hadhara katika Kata ya Segese.
Mbali na mikutano hiyo, Waziri Mkuu anatarajiwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo mradi wa Taasisi ya Elimu ya Ushirika na Biashara uliopo Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, pamoja na ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama.
Miradi mingine atakayotembelea ni shule ya mafunzo ya amali inayojengwa katika Halmashauri ya Ushetu na mradi wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Kahama kwenda Ulyankulu, unaotekelezwa katika Halmashauri ya Msalala.
Akizungumzia maandalizi ya ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote atakayopita Waziri Mkuu ili kupata fursa ya kumsikiliza na kushiriki katika mikutano hiyo ya hadhara.
TAFUTA HABARI
Social Plugin