Shamba la zao la mikorosho katika kijiji cha Angalia kata ya Mtina Tarafa ya Lukumbule Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma 
Na Regina Ndumbaro, Tunduru-Ruvuma
Wakulima wa zao la korosho katika Kijiji cha Angalia, Kata ya Mtina, Tarafa ya Lukumbule, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameiomba Serikali kuwawezesha kupata mikopo itakayowasaidia kugharamia shughuli za kilimo, hususan palizi na ununuzi wa viuatilifu, ili kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa zao hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mnada wa nne wa zao la korosho uliofanyika kupitia Chama cha Msingi cha Ushirika cha Mshikamano AMCOS, wakulima hao wamesema ukosefu wa mitaji umekuwa changamoto inayowakwamisha kuhudumia mashamba yao ipasavyo, licha ya kuwa na maeneo makubwa yanayoweza kuongeza uzalishaji endapo yatatunzwa vizuri.
Mkulima Simba Kakole amesema Serikali inapaswa kuwapa wakulima kipaumbele katika upatikanaji wa mikopo, hasa kipindi cha palizi, ili kuwawezesha kuhudumia mashamba yao kwa wakati na kuongeza uzalishaji wa korosho.
Amesema baadhi ya wakulima, hasa wenye umri mkubwa na mashamba mengi, wanashindwa kuyahudumia kutokana na kukosa nguvu kazi na uwezo wa kifedha, hali inayowalazimu kukodisha baadhi ya mashamba yao kwa makubaliano ya muda wa miaka mitano ili kupata fedha za kuhudumia mashamba mengine.
Ameeleza kuwa hatua hiyo haichukuliwi kwa hiari ya wakulima, bali ni matokeo ya changamoto za kiuchumi zinazowakabili, hivyo mikopo yenye masharti rafiki inaweza kuwasaidia kuendelea kumiliki na kuhudumia mashamba yao badala ya kuyakodisha kwa kukosa uwezo.
Aidha, amesema changamoto nyingine ipo katika upuliziaji wa viuatilifu, akibainisha kuwa mkulima anaweza kuwa na mifuko miwili ya salfa na chupa tatu au nne za dawa huku akiwa na mashamba yenye ukubwa wa ekari nne au tano.
Hali hiyo humlazimu kufanya upuliziaji mara mbili au tatu pekee na kushindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa fedha za kununua dawa za kutosha.
Amesema baadhi ya wakulima hulazimika kuzungushia mipaka mashamba ambayo hawajaweza kuyapulizia ili kuyalinda dhidi ya kuungua moto, huku akipongeza bei ya korosho ya mwaka huu kuwa nzuri na nafuu ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Ameongeza kuwa mfumo wa kuwawezesha wakulima kiuchumi unapaswa kuendelea kuboreshwa ili kuwasaidia wenye mashamba makubwa kuyahudumia na kuepuka changamoto zinazoweza kuwafanya washawishiwe kukodisha mashamba yao kwa watu wengine.
Kwa upande wake, mkulima Hongera Mussa Athumani ameiomba Serikali kupitia vyama vya ushirika kuhakikisha wakulima wanapatiwa viuatilifu vyenye ubora na viwango vinavyokidhi mahitaji ya zao la korosho ili kuongeza uzalishaji.
Amesema kumekuwepo na changamoto ya maua ya mikorosho kukauka, hali ambayo imeathiri uzalishaji wa mwaka huu ikilinganishwa na matarajio ya wakulima, huku akibainisha kuwa kuna tofauti kati ya matokeo ya uzalishaji wa mwaka uliopita na mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, ameiomba Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) kuhakikisha kinawapatia wakulima viuatilifu bora vinavyoweza kusaidia kukabiliana na changamoto hizo na kuimarisha uzalishaji wa korosho.
Akizungumzia changamoto hizo, Afisa Ushirika wa Wilaya ya Tunduru, Rashidi Maengo, amewataka wakulima wa Mshikamano AMCOS kuendelea kuzingatia ubora wa korosho wanazozalisha na kuzipeleka kwenye minada, akisema bei nzuri inayopatikana inachangiwa na ubora wa mazao yanayokusanywa.
Maengo amesema wakulima wanapaswa kuhakikisha wanarejesha magunia ya vyama vya ushirika kwa wakati na kutumia magunia husika wakati wa kupima korosho zao ili kuepuka kujipunguzia wenyewe kiasi cha mazao wanachostahili kulipwa.
Aidha, amewataka wakulima kuepuka kutumia akaunti za benki za watu wengine kupokea malipo ya korosho, akisisitiza kuwa kila mkulima anapaswa kuwa na akaunti yake ili kuhakikisha fedha zinamfikia mhusika halali na kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza.
Amefafanua kuwa wakulima wanapaswa kuwasilisha namba za akaunti zao badala ya namba za kadi za benki, huku akiwapongeza kwa kufanikisha mnada huo wa nne bila changamoto yoyote.
Akihitimisha mnada huo, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU), Musa Manjaule, amesema mnada wa nne umeuza jumla ya kilo 3,582,703 za korosho, ambapo bei ya juu ilikuwa Sh3,320 kwa kilo, bei ya chini Sh3,180 na bei ya wastani Sh3,273, huku bei ya wastani ikiwa imeongezeka kwa Sh58 ikilinganishwa na mnada uliotangulia.
Manjaule amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Angalia kwa juhudi zao katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo, akisema wameonyesha uwezo mkubwa wa kuzalisha si korosho pekee bali pia mazao mengine.
Pia amekipongeza Chama cha Mshikamano AMCOS kwa kuvuka changamoto mbalimbali na kuendelea kusimama imara, huku akisisitiza kuwa msingi wa maendeleo ya ushirika ni uaminifu na uadilifu.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa wakulima kuhakikisha wanarejesha magunia ya vyama vya ushirika yakiwa na korosho na kuonya dhidi ya vitendo vya wizi wa magunia hayo.
Amesema korosho zinapohifadhiwa kwa muda mrefu ubora wake hupungua, hivyo ni muhimu kuhakikisha zinakusanywa na kuuzwa kwa wakati.
Aidha, Manjaule amewahimiza wakulima kuanza kuzingatia matumizi ya mbegu za kisasa za mikorosho, akisema matokeo ya tafiti yanaonesha kuwa aina hizo za mikorosho zinafanya vizuri katika uzalishaji.
Ameshauri wakulima wenye mashamba makubwa, kuanzia ekari tano, 20 na kuendelea, kutenga sehemu ya mashamba yao kwa ajili ya kupanda mikorosho ya kisasa ili kuweza kulinganisha matokeo yake na mikorosho ya kienyeji na kujionea tofauti ya uzalishaji.
Amesema hatua hiyo itawasaidia wakulima kujiridhisha kwa vitendo kuhusu aina ya mikorosho inayofanya vizuri zaidi na hatimaye kufanya maamuzi sahihi yatakayochochea ongezeko la uzalishaji na maendeleo ya zao la korosho wilayani Tunduru.


TAFUTA HABARI
Social Plugin