▪ Ataka walimu wawili waliojitolea kwa zaidi ya miaka mitano waajiriwe kutokana na mchango wao katika ufaulu
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amevitaka vikundi vya Sungusungu kutowatenga wananchi wala kuwalazimisha kushiriki taratibu zinazokinzana na imani zao, akionya kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha mgawanyiko katika jamii.
Ametoa maelekezo hayo leo (Jumanne, Novemba 10, 2026), wakati akisikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Singita, Kata ya Usanda, Jimbo la Itwangi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
“Kama mtu imani yake haimruhusu kuchanja, kwa kweli tusimlazimishe. Na wala tusimtenge,” amesema.
Maelekezo hayo yamefuatia malalamiko ya mwananchi, Simon John, aliyedai kuwa mchungaji wake ametengwa baada ya kukataa kushiriki baadhi ya taratibu za Sungusungu, huku waumini wakizuiwa kwenda kusali kwake.
Akizungumza na kiongozi wa Sungusungu aliyekuwapo mkutanoni, Waziri Mkuu amemtaka kuhakikisha mchungaji huyo hatengwi na anaendelea kupewa ulinzi.
“Msisumbuane na mchungaji mmoja huyo. Mpeni na ulinzi, wala msimtenge,” amesema.
Dkt. Mwigulu ameelekeza vikundi vya Sungusungu kuwaruhusu waumini, wakiwemo wanachama wa vikundi hivyo, kwenda kusali kwa mchungaji huyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa imani na ibada.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema atamwandikia Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais–Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili walimu wawili wa kujitolea waliochangia Shule ya Msingi Masunula kushika nafasi ya pili kitaifa waajiriwe.
Shule hiyo ipo Kijiji cha Masunula, Kata ya Usule, wilayani Shinyanga. Amesema ameelezwa kuwa walimu hao wamefundisha kwa kujitolea kwa zaidi ya miaka mitano katika shule hiyo yenye walimu saba.
“Hawa waajiriwe kwa sababu tumeona matokeo yake,” amesema.
Amewapongeza walimu, wanafunzi na viongozi kwa mafanikio hayo, huku akielekeza tathmini ya gharama za ujenzi wa nyumba yenye makazi ya walimu wawili ifanyike na kuwasilishwa kupitia Katibu Tawala wa Mkoa ili kupunguza changamoto ya makazi katika shule hiyo.
Kuhusu huduma za afya, Waziri Mkuu amemwelekeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga kuwasilisha siku hiyo hiyo maombi maalumu ya ujenzi wa vituo viwili vya afya katika kata za Usule na Didia.
Vilevile, ameahidi kutafuta shilingi milioni 76 za kukamilisha Zahanati ya Mwamkanga ili wananchi waanze kupata huduma.







TAFUTA HABARI
Social Plugin