Na Dotto Kwilasa, Dodoma
WAKATI gharama za nishati ya kupikia zikiendelea kuwa sehemu ya matumizi muhimu ya kaya nyingi nchini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeingia kuongeza ushindani katika soko la nishati hiyo kwa kupanua uzalishaji wa mkaa mbadala wa Rafiki Briquette.
Hatua hiyo imekuja baada ya shirika hilo kuzindua kiwanda chake kipya jijini Dodoma, ambacho ni cha nne tangu kuanza kwa uzalishaji wa bidhaa hiyo inayotokana na makaa ya mawe.
Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Mkaa huo una uwezo wa kuwaka kwa zaidi ya saa tatu na nusu, huku kilo moja ikiuzwa kwa Sh1,000, jambo linaloweka mjadala kuhusu nafasi ya bidhaa hiyo katika kupunguza gharama za nishati ya kupikia kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho Leo November 7,2026 Chigongwe Jijini Dodoma,Waziri huyo alisema STAMICO inapaswa kuhakikisha bidhaa hiyo haibaki katika maeneo ya uzalishaji pekee, bali inasambazwa kwa wingi na kupatikana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha amelielekeza shirika hilo kuimarisha mfumo wa masoko kwa kushirikiana na wafanyabiashara na mawakala, akisisitiza kuwa jukumu la uzalishaji linapaswa kwenda sambamba na mikakati madhubuti ya kuwafikia watumiaji.
Amesema matumizi ya nishati hiyo ni sehemu ya mchango wa sekta ya madini katika kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameitaka STAMICO kutumia fursa ya rasilimali za madini ilizonazo kupanua uwekezaji, akieleza kuwa shirika hilo sasa linaendelea na miradi mbalimbali ikiwemo dhahabu Kigosi, madini ya kimkakati Morogoro na nikeli Mtwara.
Akizungumzia mabadiliko ya shirika hilo, alisema STAMICO ambalo miaka mitano iliyopita lilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyotathminiwa kwa uwezekano wa kufutwa kutokana na kutokuwa na tija, sasa limefikia mapato ya zaidi ya Sh bilioni 89 kutoka Sh milioni moja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse amesema kiwanda cha Dodoma kimejengwa kwa kuzingatia nafasi ya mji huo kama makao makuu ya nchi na mahitaji ya nishati safi katika mkoa huo na maeneo jirani.
Amesema shirika limejenga mtandao wa mawakala 92 nchini, wakiwemo 35 kutoka taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania, ili kurahisisha usambazaji wa bidhaa hiyo.
Amesema katika uzinduzi huo wamekabidhi pia magari madogo aina ya toyo 30 na kontena kwa ajili ya kuwezesha usafirishaji na uuzaji wa Rafiki Briquette katika maeneo mbalimbali.
Dkt. Mwasse amesema wazo la kuzalisha bidhaa hiyo lilitokana na utafiti ulioanza mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2022, huku bidhaa hiyo ikipata cheti cha ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Ameongeza kuwa shirika linaendelea na maandalizi ya kiwanda kingine mkoani Geita ili kuongeza uzalishaji na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Mbali na uwekezaji katika nishati safi, amesema STAMICO imeagiza mitambo 10 ya uchorongaji madini kwa lengo la kuimarisha shughuli za utafiti na kuongeza ajira kwa vijana.
Amesema kila mtambo mmoja unatarajiwa kutoa ajira kwa vijana takribani 50, hivyo mitambo yote ikifanya kazi itatoa fursa za ajira kwa vijana takribani 500.
Naye mwakilishi wa taasisi ya Wanawake na Samia Tanzania Fatma Madidi alisema wanawake wamepata fursa ya kuwa mawakala wa bidhaa hiyo katika maeneo mbalimbali nchini na wamejipanga kuhakikisha inawafikia watumiaji wengi zaidi.
Amesema STAMICO imewawezesha kupata kontena na vifaa vya usafirishaji, hatua itakayowasaidia kushiriki katika biashara ya nishati safi na kuchangia utekelezaji wa lengo la taifa la matumizi ya nishati safi ifikapo mwaka 2034.








TAFUTA HABARI
Social Plugin