Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHULE ZA BWENI KAGERA ZATAKIWA KUANGAMIZA KUNGUNI NA VIROBOTO KABLA YA DESEMBA 20

Na Mbuke Shilagi Kagera.


Afisa Afya wa Mkoa wa Kagera Bw. Yasin Mwinory amezitaka halmashauri zote nane za mkoa huo kuhakikisha shule zote za bweni zinafanya usafi wa kina na kupulizia dawa za kuangamiza wadudu waharibifu kabla ya Desemba 20 mwaka huu, kwa lengo la kulinda afya na usalama wa wanafunzi.


Agizo hilo linahusisha udhibiti wa wadudu mbalimbali wakiwemo kunguni na viroboto, ambao wanaweza kuhatarisha afya za wanafunzi wanapoishi katika mazingira yasiyo safi.


Akitoa maelekezo hayo, Mwinory amesema hatua hiyo inazingatia Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009, kifungu cha 71, kinachowataka wamiliki wa maeneo yenye mikusanyiko ya watu kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na yanafanyiwa udhibiti wa wadudu waharibifu.


Aidha, amewataka wamiliki wa shule kuhakikisha mabweni na vitanda vinapakwa rangi upya, pamoja na kufanya usafi wa mara kwa mara ili kuzuia wadudu hao kuzaliana na kuenea.


Amesisitiza kuwa shule zinapaswa kuzingatia usafi wa mazingira kama sehemu muhimu ya kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora na salama ya kuishi na kujifunzia.


Kwa mujibu wa agizo hilo, ifikapo Desemba 20, maafisa afya wa halmashauri zote wanapaswa kuwasilisha taarifa za shule zilizotekeleza maelekezo hayo pamoja na zile ambazo zitakuwa hazijatekeleza.


Hatua hiyo inalenga kuhakikisha shule zote za bweni zinakuwa katika mazingira yanayokidhi viwango vya afya na usalama kabla ya kuendelea kupokea wanafunzi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com