Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SGR MAKUTUPORA–TABORA IKAMILIKE MWAKA HUU - BALOZI OMARI



Na Sheila Ahmadi, Tabora

Serikali imewataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR)kipande cha Makutupora hadi Tabora mkoani Tabora ili kuongeza kasi ya kazi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa.

Wito huo umetolewa Mkoani Tabora na Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omari wakati wa ziara ya pamoja na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika eneo la Tura mkoani Tabora.

Balozi Omari amesema Serikali inatarajia mradi huo kukamilika ndani ya mwaka huu hivyo ni muhimu kwa kuwa wakandarasi Wanaongeza juhudi na kasi ya utekelezaji ili kuruhusu reli hiyo kuanza kutoa huduma kwa wananchi na kuchochea mageuzi katika sekta ya usafiri nchini.

Aidha wakandarasi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuzingatia muda wa utekelezaji huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi na kuhakikisha rasilimali zinazohitajika zinapatikana ili mradi huo ukamilike kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema mradi huo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuleta mageuzi katika sekta ya uchukuzi kwa kuboresha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo.

Aidha Serikali itaendelea kushirikiana na wakandarasi kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi huo, ili kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kasi inayohitajika na kukamilika kwa wakati.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Machibya Shiwa ameongeza kuwa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ulioanza mwaka 2022 hatua inayolenga kuhakikisha ujenzi unaendelea na kukamilika kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com