Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTENDAJI MKUU TANROADS ENG BESTA ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA BARABARA YA NJIA NNE MBEYA


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara ya njia nne jijini Mbeya, ambao hadi sasa umefikia asilimia 47.3 ya utekelezaji wake.

Mhandisi Besta ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo, unaohusisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 29, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia utekelezaji wake ili ukamilike kwa viwango na muda uliopangwa.

Katika ziara hiyo, amewatoa hofu wananchi ambao nyumba zao 10 zimepitiwa na mradi huo, akiwahakikishia kuwa watalipwa fidia ya takribani shilingi milioni 400. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha wananchi hao wanapata haki yao kwa wakati.

Akizungumzia mradi huo, Mhandisi Besta amesema maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, kuhusu ujenzi huo yanaendelea kutekelezwa. Amesema kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo ni miongoni mwa sababu zilizomfanya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya kazi.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Suleiman Bishanga, amesema ujenzi wa barabara hiyo ya kilomita 29 umefikia asilimia 47.3, huku akiwashukuru viongozi kwa kuendelea kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Nzovwe, Gideon Shiyo, amesema wanafurahishwa na ujenzi wa barabara hiyo, huku akiomba fidia ilipwe kwa wakati kwa wananchi ambao nyumba zao zimepitiwa na mradi huo.

Naye Maria amesema ujenzi wa mitaro na mifereji ya maji umesaidia kutatua changamoto zilizokuwepo katika eneo la biashara la Eso, ambako wananchi wamekuwa wakifanya shughuli zao za kujipatia kipato.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com