
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Deogratus Ndejembi akisalimiana na wabunge wa Jimbo la Tunduru mkoani Ruvuma na viongozi wengine baada ya kuwasili katika mradi wa kimkakati wa umeme wa kilovoti 220 kutoka Songea kupitia Tunduru hadi Masasi pamoja na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya msongo wa kilovoti 220/33 katika wilaya za Tunduru na Masasi
Na Regina Ndumbaro, Ruvuma
MRADI wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea kupitia Tunduru hadi Masasi, pamoja na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya msongo wa kilovoti 220/33 katika wilaya za Tunduru na Masasi, umeibua matumaini makubwa kwa wananchi wa Kanda ya Kusini wanaotarajia kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
Mradi huo wa kimkakati unaotekelezwa na kampuni ya Kalpataru Projects International Limited kutoka nchini India, ukiwa chini ya usimamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), umekuwa miongoni mwa miradi inayotazamwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.
Hata hivyo, matumaini hayo ya wananchi yameambatana na msisitizo wa Serikali kuhusu umuhimu wa kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, kuonesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wake wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo wilayani Tunduru, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Ruvuma.
Akizungumza mbele ya hadhira wakati wa ziara hiyo, Mhe. Ndejembi amemtaka mkandarasi anayesimamia utekelezaji wa mradi huo, Neeraj Singh, kuongeza kasi ya kazi na kuhakikisha ahadi alizozitoa zinatekelezwa, akieleza kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha malipo ya mkandarasi yanafanyika kwa wakati ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa wananchi.
Amesema Serikali inatarajia kuona matokeo yanayoendana na dhamira ya uwekezaji huo, akisisitiza kuwa wananchi wa Tunduru wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kukatika kwa umeme mara kwa mara na kwamba mradi huo unapaswa kuwa miongoni mwa suluhisho la changamoto hiyo. Amesema: “Uliahidi kutekeleza, lakini hakuna nilichoridhika nacho katika kile ninachokiona kwa mkandarasi huyu. Mradi huu ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Tunduru kupunguza kabisa changamoto zinazowakabili za umeme kukatika mara kwa mara. Tukiendelea hivi hatutafika.”
Kauli hiyo imekuja wakati wananchi wa Tunduru wakiwa na matarajio makubwa ya kuona mradi huo unakamilika, kutokana na athari wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku, zikiwemo biashara, uzalishaji mali, huduma za kijamii na shughuli zinazotegemea matumizi ya umeme.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa mradi huo, mkazi wa Tunduru, Abdulkader Issa, amepongeza ziara ya Makamu wa Rais, akisema uwepo wake wilayani humo ni jambo kubwa kwa wananchi kwa kuwa umetoa fursa ya kushuhudia na kufuatilia utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
Amesema mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi, kwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuvutia wawekezaji na kutoa fursa zaidi za uzalishaji na biashara.
Ameeleza kuwa wananchi wa Kanda ya Kusini wamekuwa na kilio cha muda mrefu kuhusu changamoto ya umeme, hivyo uwekezaji huo unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni hatua muhimu katika kuharakisha maendeleo ya eneo hilo.
Aidha, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiona Kanda ya Kusini katika mipango ya maendeleo, huku akiwataka Watanzania kuwaombea viongozi wanaotekeleza majukumu ya kuwatumikia wananchi na kuendelea kudumisha amani ya nchi, akisisitiza kuwa pale changamoto zinapojitokeza, wananchi wanapaswa kufuata sheria na kuviachia vyombo husika kushughulikia masuala yanayowahusu badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Kwa upande wake, mkazi mwingine wa Tunduru, Zainab Mwenda Chale, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi huo, huku akiiomba Serikali na mkandarasi kuhakikisha kazi zinafanyika kwa kasi ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika.
Amesema changamoto ya kukatika kwa umeme imekuwa ikiathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi, hususan wakati wananchi wanapopeleka mahindi kwenye mashine za kusaga, hali inayosababisha kusubiri kwa muda mrefu na wakati mwingine kupata hasara kutokana na kuharibika kwa vifaa vya umeme majumbani.
Ameongeza kuwa tatizo hilo linaathiri pia upatikanaji wa huduma ya maji kwa kuwa baadhi ya mifumo ya kusukuma na kusambaza maji inategemea nishati ya umeme, hivyo kuwa na umeme wa uhakika kutarahisisha upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Amesema: “Tunaiomba Serikali na mkandarasi anayesimamia mradi huu kuhakikisha unatekelezwa haraka ili tuondokane na changamoto hizi. Tunapopeleka mahindi kwenye mashine za kusaga, umeme unapokatika tunalazimika kusubiri kwa muda mrefu, wakati mwingine vifaa vya umeme majumbani vinaharibika na kutusababishia hasara. Hata huduma ya maji inategemea umeme, hivyo umeme ukiwa wa uhakika kila kitu tutakipata kwa urahisi.”
Kwa ujumla, utekelezaji wa mradi huo wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Songea kupitia Tunduru hadi Masasi, pamoja na vituo vya kupoza umeme vya kilovoti 220/33 vya Tunduru na Masasi, unabeba matarajio ya wananchi ya kupata huduma bora ya umeme, kukuza shughuli za uzalishaji na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika Kanda ya Kusini.
Hata hivyo, msisitizo wa Makamu wa Rais kuhusu kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaonesha kuwa matarajio ya wananchi yanahitaji kuambatana na hatua madhubuti kutoka kwa mkandarasi ili uwekezaji huo mkubwa uweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa na Serikali na manufaa halisi kwa wananchi.




TAFUTA HABARI
Social Plugin