Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIJESHI KUHAKIKISHA AMANI AFRIKA




Na mwandishi wetu,Arusha

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na usalama wa pamoja barani Afrika, ikieleza kuwa mafunzo ya kitaaluma na kubadilishana uzoefu baina ya majeshi ni nguzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazozikabili nchi za Afrika.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema hayo Novemba 11, 2026, jijini Arusha wakati akifunga rasmi Mkutano wa 20 wa Makamanda wa Vyuo vya Ukamanda na Mafunzo ya Kijeshi barani Afrika (African Conference of Commandants – ACoC).

Katika hotuba yake, Dkt. Nyansaho aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa washiriki wote wa mkutano huo.

Aliwapongeza makamanda na wajumbe kwa ushiriki na michango yao katika kuimarisha elimu ya kijeshi na kukuza ushirikiano baina ya taasisi za kijeshi barani Afrika.

Alisema elimu na mafunzo ya kitaaluma ya kijeshi yana nafasi muhimu katika kuandaa viongozi wenye maarifa, maono na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazozikabili nchi za Afrika, zikiwemo ugaidi, uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka ya nchi na vitisho vya kimtandao.

Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano baina ya vyuo vya kijeshi kupitia mafunzo ya pamoja, kubadilishana wanafunzi na wakufunzi pamoja na kuoanisha mitaala ya mafunzo ya kijeshi.

Alitaja maeneo muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele kuwa ni Operesheni za Kusaidia Amani, Sheria za Kimataifa za Kibinadamu na Ulinzi wa Raia, akieleza kuwa ushirikiano katika maeneo hayo utaongeza uwezo wa majeshi ya Afrika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Mkutano huo uliwakutanisha viongozi waandamizi wa kijeshi na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, akiwemo Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salumu Haji Othman; Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Tanzania na Mwenyekiti wa Mkutano wa Makamanda wa Vyuo vya Kijeshi vya Afrika (ACoC), Meja Jenerali Stephen Justice Mnkande; pamoja na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele.

Wengine walioshiriki ni wawakilishi wa Umoja wa Afrika, makamanda wa vyuo vya kijeshi, wakufunzi wakuu na maafisa waandamizi wa kijeshi kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Mkutano huo umekuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za mafunzo ya kijeshi, kwa lengo la kujenga uwezo wa pamoja wa majeshi ya Afrika na kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama.

Hatua hiyo inalenga kuchangia juhudi za pamoja za nchi za Afrika katika kudumisha amani, usalama na utulivu wa kudumu barani humo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com