Na Sheila Ahmadi, Dar es salaam
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amezitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha barabara maalumu zinazounganisha eneo la Kurasini Logistic Park zinakamilishwa kwa haraka ili kuruhusu eneo hilo kuanza kutoa huduma kwa wakati.
Profesa Mbarawa ametoa maelekezo hayo wakati wa kutembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam kupitia Kurasini Logistic Park ambapo amesema kuwa mradi huo ni sehemu muhimu ya uwekezaji unaolenga kuongeza uwezo wa bandari katika kuhudumia shehena na kupunguza msongamano.
mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi makasha 150,000, huku awamu ya pili ikiwa na uwezo wa kuhifadhi makasha 550,000 kwa mwaka hivyo kufanya eneo lote kuwa na uwezo wa kuhifadhi makasha 700,000 kwa mwaka.
Aidha kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa baadhi ya taratibu za ukaguzi wa makasha ikiwemo uhakiki wa nyaraka na ukaguzi wa kutumia vifaa maalumu vya uchunguzi (scanning) zitafanyika katika eneo hilo.
"Utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya uwekezaji unaofanywa na sekta binafsi ambapo mwekezaji anayetekeleza mradi huo pia amepewa dhamana ya kuendesha Kituo cha Huduma za Makasha Namba Mbili (Terminal Two) hatua inayochochea upanuzi na uboreshaji wa huduma za bandari."Amesema Profesa Mbarawa".
Hata hivyo ushirikiano kati ya TPA, TANROADS na TARURA ni muhimu katika kuhakikisha miundombinu ya barabara inayohitajika inakamilishwa kwa wakati ili kurahisisha usafirishaji wa makasha kwenda na kutoka eneo hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bandari ya Daresalaam Abed Gallus Abed ameongeza kuwa ongezeko la shehena katika Bandari ya Dar es Salaam limeongeza uhitaji wa maeneo ya kuhifadhi makasha, hivyo kukamilika kwa Kurasini Logistic Park kutasaidia kukabiliana na changamoto hiyo.
mwaka uliopita bandari ilihudumia zaidi ya makasha milioni 1.3 huku mwaka huu ikitarajiwa kuhudumia zaidi ya makasha milioni 1.5 hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza uwezo wa miundombinu ya kuhifadhi na kuhudumia shehena.
Katika Hatua nyingine Mkurugenzi Abed amesema eneo hilo litakuwa na vifaa vya kutosha vya scanning na mifumo ya uhakiki wa makasha, ambapo taratibu hizo zitasaidia kupunguza msongamano unaotokana na ukaguzi unaofanyika ndani ya bandari na kuongeza kasi ya mtiririko wa shehen
a.



TAFUTA HABARI
Social Plugin