Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAFUTA KODI YA SARUJI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara wenye lengo la kufuatilia, kukagua utekelezaji wa miradi na utoaji huduma kwa wananchi wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Novemba 8,2026 viwanja vya SHIRECU

Na Sumai Salum-Kishapu


WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imefuta kodi kwenye saruji inayoingizwa kutoka nje ya nchi pamoja na malighafi zinazotumika kutengeneza saruji, hatua inayolenga kupunguza gharama za ujenzi na kushusha bei ya bidhaa hiyo nchini.


Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Novemba 8, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga.


Amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya Serikali kubaini ongezeko la bei za vifaa vya ujenzi, akibainisha kuwa wananchi wanapaswa kutarajia kushuka kwa bei ya saruji siku zijazo, huku Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kudhibiti gharama za vifaa vingine muhimu vya ujenzi.


Katika hatua nyingine, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia matumizi ya dawa katika hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati nchini, baada ya kubaini kuwepo kwa malalamiko ya wananchi kukosa dawa katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma licha ya taarifa za Serikali kuonesha kuwa na utoshelevu wa dawa kwa asilimia 97 kwa 96.


Amesema Serikali haiko tayari kuona baadhi ya watumishi wasio waadilifu wakihujumu juhudi za Rais katika kuboresha huduma za afya, huku akimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (RMO) kuwafikishia maelekezo hayo watendaji walio chini yake ili kuhakikisha dawa zinapatikana na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.


“Baadhi ya hospitali zinapokea fedha na kutoa taarifa za utoshelevu wa dawa kwa asilimia 97 na 96, lakini mgonjwa anapokwenda kupata huduma anaambiwa hakuna dawa na aende kununua kwenye maduka ya nje. Je, kuna michezo inayofanyika?” amehoji.


Amesisitiza kuwa Serikali haitakubali uzembe kuwa sheria, utaratibu wala mazoea, akieleza kuwa imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya kwa kujenga zaidi ya Hospitali 100 za Wilaya, Vituo vya afya 600 na Zahanati 2,700, pamoja na kununua magari ya kisasa ya kubebea wagonjwa wa dharura ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com