Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMANDA MAGOMI ATOA WITO KWA WAZAZI NA WALEZI KUSHIRIKIANA NA JESHI LA POLISI KATIKA MALEZI YA WATOTO


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, amewataka wazazi na walezi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kusimamia malezi bora na maadili ya watoto ili kuwajenga katika misingi mizuri ya kijamii.

Kamanda Magomi ametoa wito huo alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 12 ya kuhitimu Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Francis wa Assisi, iliyopo Manispaa ya Shinyanga.

Amesema wazazi na walezi wanapaswa kutimiza wajibu wao wa malezi kwa kuwashauri, kuwaonya na kuwakemea watoto wanapokosea, badala ya kuwaogopa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwajenga katika maadili mema.

Aidha, amewataka wahitimu kuhakikisha wanadumisha maadili waliyojifunza shuleni hata wanaporejea katika familia na jamii zinazowazunguka, na kujiepusha na tabia zisizofaa ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili.

Vilevile, amewataka wahitimu kuzingatia misingi sahihi ya kijamii na kuishi kwa kuzingatia kaulimbiu ya shule hiyo inayosema “Imani, Maarifa na Huduma.”

Katika hatua nyingine, Kamanda Magomi amechangia kiasi cha shilingi milioni moja (TSh 1,000,000) ikiwa ni sehemu ya harambee ya kuchangia ujenzi wa kisima cha maji katika shule hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com