Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE ABUBAKARI OMARI ATOA WITO KWA WAZAZI KUWALINDA WATOTO WAKATI WA LIKIZO


Mbunge wa Jimbo la Manonga, Mhe. Abubakari Alli Omari.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mbunge wa Jimbo la Manonga, Mhe. Abubakari Alli Omari, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawalinda na kuwafuatilia watoto wao katika kipindi hiki cha likizo ya shule, akisisitiza umuhimu wa kuwalea katika maadili mema na kuwaepusha na makundi hatarishi yanayoweza kuathiri maisha yao.

Katika ujumbe wake alioutoa kwa wananchi wa Jimbo la Manonga na Watanzania kwa ujumla, Mbunge huyo amesema kipindi cha likizo ni wakati muhimu kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao, kuwafuatilia mienendo yao na kuhakikisha wanatumia muda wao katika shughuli zenye manufaa.

Amesema wazazi hawapaswi kuwaacha watoto wazurure mitaani bila uangalizi, bali wanapaswa kuwajua marafiki zao, maeneo wanayokwenda na shughuli wanazofanya ili kuwakinga dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha na mustakabali wao.

Mhe. Omari amewataka wazazi kuwa makini na mienendo ya watoto wao ili wasijiingize katika makundi yasiyofaa yanayoweza kuwashawishi kujihusisha na vitendo kama ulevi, uvutaji wa sigara, wizi na tabia nyingine zinazokwenda kinyume na maadili mema ya jamii.

Amesisitiza kuwa watoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuhakikisha wanapata malezi bora, ulinzi na mwongozo unaowawezesha kukua katika mazingira salama.

Aidha, amewahimiza wazazi kuitumia fursa ya likizo kuwa karibu zaidi na watoto wao kwa kuwafundisha maadili mema, kuwajengea tabia ya kufanya kazi, kuwapa elimu ya maisha pamoja na kuwalea katika misingi ya kumcha Mungu.

Amesema malezi ya watoto yanahitaji ushirikiano na uwajibikaji wa wazazi na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha kizazi kinachokua kinakuwa na nidhamu, maadili na uwezo wa kuchangia maendeleo ya familia na taifa.

Katika ujumbe huo, Mbunge huyo pia amewaombea Watanzania kuendelea kudumisha umoja na amani, huku akimwomba Mwenyezi Mungu kuibariki Tanzania na kuwalinda watoto wote katika kipindi hiki cha likizo.

Amehitimisha ujumbe wake kwa kuwatakia wananchi Ijumaa yenye baraka, akisisitiza upendo na mshikamano kwa wananchi wa Jimbo la Manonga kupitia salamu zake za “Manonga One!”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com