
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, katika ukumbi wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Novemba 12, 2026. Picha na Kadama Malunde
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, katika ukumbi wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Novemba 12, 2026.
Na Kadama Malunde - Shinyanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kusaidia kurejeshwa kwa jumla ya Shilingi 236,069,957.63 katika kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, kufuatia hatua mbalimbali za uchunguzi, ufuatiliaji wa ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.
Hayo yameelezwa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Mwamba Masanja, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba 2026, katika ukumbi wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Novemba 12, 2026.
Masanja amesema fedha hizo zimepatikana kupitia operesheni na ufuatiliaji uliofanywa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya halmashauri, malipo ya ushuru wa huduma, malipo ya wakulima wa pamba pamoja na uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma.
Amesema kati ya fedha hizo, Shilingi 75,500,500 zilirejeshwa baada ya TAKUKURU kufuatilia ukusanyaji wa mapato kupitia mashine za kielektroniki za POS katika Kata ya Old Shinyanga, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.


Ameeleza kuwa ufuatiliaji huo ulibaini kuwepo kwa changamoto katika ukusanyaji na uwasilishaji wa fedha zilizokusanywa kupitia mashine hizo, ambapo baadhi ya mawakala hawakuwa wakiwasilisha fedha hizo benki kama ilivyotakiwa, hali iliyosababisha mapato ya halmashauri kutokufika kwenye mfumo rasmi wa ukusanyaji wa mapato.
Katika hatua nyingine, amesema TAKUKURU ilisaidia kurejeshwa kwa Shilingi 47,877,360 zilizohusiana na ufuatiliaji wa malipo ya wakulima wa pamba katika msimu wa 2025/2026, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.
Amesema ufuatiliaji huo ulihusisha makampuni yenye vibali vya kununua pamba kwa msimu huo pamoja na vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), baada ya kubainika kuwepo kwa malalamiko ya wakulima kuhusu malipo ya pamba waliyouza. Hatua zilizochukuliwa zilisaidia kuhakikisha wakulima waliokuwa na madai wanapata stahiki zao.
Aidha, katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, TAKUKURU ilisaidia kurejeshwa kwa Shilingi 35,129,844.63 zilizokusanywa kutoka kwa wadaiwa sugu wa ushuru wa huduma (Service Levy), ambao walikuwa wamekwepa kulipa ushuru huo kwa muda mrefu.
Masanja amesema pia taasisi hiyo ilifanikiwa kurejesha Serikalini Shilingi 74,870,114 kutokana na uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za ubadhirifu wa mali za umma, ambapo watuhumiwa walifikishwa mahakamani na kukiri makosa yao.
Ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo
Akizungumzia usimamizi wa miradi ya maendeleo, Masanja amesema TAKUKURU ilifanya ufuatiliaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu mipya katika Zahanati ya Mwakitolyo uliokuwa na bajeti ya Shilingi milioni 250.
Amesema katika ufuatiliaji huo ilibainika kutowasilishwa kwa baadhi ya malipo ya kodi ya zuio (Withholding Tax), ambapo hatua zilizochukuliwa ziliwezesha kurejeshwa kwa Shilingi 2,692,139.
Vilevile, amesema TAKUKURU ilifuatilia matumizi ya fedha katika miradi 10 ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi bilioni 27.9 katika sekta za elimu, afya, barabara, huduma za jamii na utawala, kwa lengo la kuhakikisha fedha zinatumika kulingana na malengo yaliyokusudiwa na miradi inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Malalamiko 134 ya rushwa na yasiyo ya rushwa yapokelewa
Katika eneo la uchunguzi wa malalamiko, Masanja amesema TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga ilipokea jumla ya malalamiko 134 katika kipindi hicho, ambapo 105 yalihusu tuhuma za rushwa na 29 yalikuwa malalamiko mengine yasiyo ya rushwa.
Amesema katika kipindi hicho, taasisi hiyo ilifungua kesi mpya 13 mahakamani, huku kesi saba zikitolewa uamuzi na kati ya hizo Jamhuri ikishinda kesi sita.
Ameeleza kuwa hatua hizo ni sehemu ya jitihada za TAKUKURU katika kuhakikisha vitendo vya rushwa vinadhibitiwa na wanaohusika wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
TAKUKURU yaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa
Masanja amesema TAKUKURU itaendelea kuimarisha mikakati ya kuzuia rushwa kwa kuongeza elimu kwa umma, kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma na kusimamia ukusanyaji wa mapato katika taasisi za umma.
Amesema taasisi hiyo pia itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kubaini mianya ya rushwa na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila kulazimika kutoa au kupokea rushwa.
Amewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Aidha, amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushirikiano wa kila mmoja, kwani rushwa inakwamisha maendeleo, inadhoofisha utoaji wa huduma na kuathiri ustawi wa jamii.
Wananchi wanaweza kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia namba ya simu 113 bila malipo.







TAFUTA HABARI
Social Plugin