WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Serikali inatarajia kutumia Shilling trilioni 89.3 kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2027/28, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuchangia Sh trilioni 62.3, sawa na sehemu kubwa ya fedha zinazohitajika.
Akiwasilisha mapendekezo ya mpango huo Bungeni jijini Dodoma, Oktoba 27, 2026, Prof. Mkumbo amesema Serikali inakusudia kutumia mpango huo kuimarisha uchumi, kuongeza ajira, kukuza uwekezaji, kuboresha huduma za jamii na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema kati ya Shilling trilioni 89.3 zinazohitajika, Sh trilioni 20.7 zinatarajiwa kutoka katika bajeti ya Serikali, Sh trilioni 6.3 kutoka kwenye uwekezaji wa mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara na Sh trilioni 62.3 kutoka sekta binafsi.
Prof. Mkumbo, amesema pia utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31), unaolenga kutafsiri malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika miradi na matokeo yanayopimika.
"Dira 2050 haitafanikiwa kwa kuwepo kwa nyaraka na mipango pekee, bali kwa utekelezaji wenye nidhamu, matumizi bora ya rasilimali, uwekezaji wenye tija na uwajibikaji wa taasisi zinazohusika". Amesisitiza Prof. Mkumbo
Katika hatua nyingine, Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa ajira mpya hadi wastani wa milioni 1.7 mwaka 2027, kutoka ajira 981,000 zilizozalishwa mwaka 2025, kupitia utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo na uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
Prof. Mkumbo amesema mpango huo utaweka msisitizo katika kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, kuongeza tija katika uzalishaji, kupanua minyororo ya thamani na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa uzalishaji, huku ikihamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa, mitambo na ubunifu ili kuongeza uwezo wa biashara na viwanda vya ndani kushindana katika masoko.
Amesema takwimu za uwekezaji zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, miradi 934 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 12.5 ilisajiliwa, ikitarajiwa kuzalisha ajira 307,743.
Aidha, katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/27, miradi 243 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.44 ilisajiliwa, huku asilimia 57.2 ya miradi hiyo ikiwa katika sekta ya viwanda.
Amesema Serikali inaendelea kutambua na kusukuma utekelezaji wa miradi 131 inayostahili kutekelezwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, hatua inayolenga kuongeza uwekezaji na kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali katika kugharamia maendeleo.
Prof. Mkumbo amesema Dira 2050 inaitambua sekta binafsi kama injini muhimu ya mageuzi ya kiuchumi, kwa kuzingatia mchango wake katika uzalishaji, ajira, biashara na mapato ya Serikali.
"sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya uwekezaji unaohitajika katika utekelezaji wa Dira 2050, huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara, kurahisisha mifumo ya udhibiti na kuimarisha ushirikiano na wawekezaji". Amesema Prof. Mkumbo
"Takwimu za utafiti wa ajira na kipato wa mwaka 2024/25 zinaonesha kuwa kati ya ajira 4,565,960 zilizobainishwa, ajira 3,220,452, sawa na asilimia 70.5, zilikuwa katika sekta binafsi". Amesisitiza Prof. Mkumbo
Amesema Serikali itaweka kipaumbele katika kuvutia uwekezaji kwenye kilimo cha maua na mazao ya bustani, ufugaji wa viumbe maji, uchimbaji na uongezaji thamani wa madini, uzalishaji wa mafuta ya kula na viwanda vya nguo na mavazi.
"Maeneo hayo yatahusisha hatua mbalimbali za minyororo ya thamani, kuanzia uzalishaji, uchakataji, uhifadhi na usafirishaji hadi kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi". Amesema Prof. Mkumbo
Katika kuimarisha huduma na miundombinu, Serikali inalenga kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme hadi megawati 4,804 ifikapo Juni 2028, kutoka megawati 4,606.14 zilizokuwepo Septemba 2026.
Aidha, kiwango cha wananchi wanaonufaika na bima ya afya kinatarajiwa kufikia asilimia 32.38 mwaka wa fedha 2027/28, kutoka makadirio ya asilimia 25 mwaka 2026/27.
"Katika sekta ya usafirishaji, Serikali inalenga kuongeza mizigo inayosafirishwa kupitia Reli ya Kati hadi tani milioni moja mwaka 2027/28, kutoka tani 810,000 zinazotarajiwa kusafirishwa mwaka 2026/27". Amesema Prof. Mkumbo
"Mchango wa bidhaa za viwandani katika mauzo yote ya nje unatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 16.9 mwaka 2027/28, kutoka asilimia 15.5 mwaka 2025". Ameongeza
Prof. Mkumbo amesema malengo hayo yanalenga kuongeza tija, kupunguza gharama za usafirishaji, kuimarisha biashara na kuongeza uwezo wa Tanzania kuuza bidhaa zenye thamani iliyoongezwa katika masoko ya kimataifa.
Prof. Mkumbo Akizungumzia vipaumbele vya kimkakati, alisema Serikali itaendeleza uwekezaji katika kilimo, viwanda, madini, mafuta na gesi, ujenzi, utalii, michezo, sanaa na ubunifu, fedha, biashara na ujasiriamali.
Katika kilimo, msisitizo utawekwa katika kukamilisha miradi ya umwagiliaji, kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha upatikanaji wa mitaji na kuimarisha viwanda vya uchakataji ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuuzwa.
Serikali pia itaendeleza mpango wa Gridi ya Taifa ya Maji kwa kutumia rasilimali za maji zilizopo katika maziwa na mito mikubwa, ikiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Mto Rufiji.
"Mpango huo hautalenga tu kuongeza upatikanaji wa maji safi, bali pia kutumia rasilimali hiyo kuchochea uzalishaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi". Amesema Prof. Mkumbo
"Katika sekta ya michezo, Serikali itaendelea na maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, huku ikiimarisha matumizi ya utalii, michezo, sanaa na ubunifu kama vyanzo vya mapato, ajira na kuitangaza Tanzania kimataifa". Ameongeza Prof. Mkumbo
Katika kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa maendeleo zinatoa matokeo yaliyokusudiwa, Prof. Mkumbo amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi, ikiwemo Mfumo wa Kitaifa wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mipango na Miradi ya Maendeleo unaojulikana kama e-Delivery.
"Mfumo huo utasaidia kufuatilia maendeleo ya miradi, matumizi ya fedha, uzingatiaji wa ratiba na hatua zinazochukuliwa kutatua changamoto zinazoweza kuchelewesha utekelezaji". Amesema Prof. Mkumbo
"Serikali haitapima mafanikio kwa idadi ya mikutano iliyofanyika au taarifa zilizoandaliwa, bali kwa huduma zilizotolewa, matokeo yaliyopatikana na maboresho halisi katika maisha ya wananchi". Amesisitiza Prof. Mkumbo
Aidha, Prof. Mkumbo amezitaka wizara, sekretarieti za mikoa, mamlaka za Serikali za mitaa na taasisi za umma ambazo bado hazijaoanisha mipango yao ya kimkakati na malengo ya Dira 2050 kufanya hivyo kabla ya Juni 2027.
"Hatua hiyo itasaidia kuhakikisha kuwa mipango ya taasisi, bajeti na miradi ya maendeleo inaendana na vipaumbele vya Taifa". Amesema Prof. Mkumbo
Akizungumzia mwenendo wa uchumi, Prof. Mkumbo amesema takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kuwa uchumi ulikua kwa asilimia 6.0 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026 na asilimia 6.5 katika robo ya pili ya mwaka huo.
Amesema uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026 na asilimia 6.6 mwaka 2027, huku Serikali ikiendelea kutekeleza sera zinazolenga kuimarisha uzalishaji, uwekezaji na biashara.
Ameongeza kuwa mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.6 katika mwaka wa fedha 2025/26, ingawa uliongezeka hadi asilimia 4.3 Septemba 2026, hali iliyochangiwa zaidi na kupanda kwa bei za nishati katika soko la dunia.
Hata hivyo, amesema mfumuko huo uliendelea kuwa ndani ya lengo la kitaifa la asilimia 3 hadi 5.
Kwa upande wa mikopo, amesema mikopo kwa sekta binafsi iliendelea kuongezeka, huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa kuelekeza mikopo hiyo katika shughuli za uzalishaji zitakazoongeza uwekezaji, ajira, mauzo ya nje na ushindani wa uchumi.
Kadhalika, Prof. Mkumbo amesema mafanikio ya Dira 2050 yatategemea maamuzi ya Serikali, rasilimali zitakazokusanywa, uimara wa taasisi na uwezo wa kutekeleza mipango kwa kuzingatia matokeo yanayopimika.
"lengo la Taifa ni kujenga Tanzania yenye ustawi unaowanufaisha wananchi wengi zaidi, ajira zenye tija, biashara zenye ushindani na huduma bora za umma". Amesema Prof. Mkumbo
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa Dira 2050 ni jukumu la pamoja linalohitaji ushiriki wa Serikali, Bunge, sekta binafsi, taasisi za elimu na utafiti, mamlaka za Serikali za mitaa, washirika wa maendeleo na wananchi.
Amesema Mafanikio ya mpango huo yatapimwa kwa namna unavyoboresha fursa za wananchi, kuongeza kipato na kuimarisha maisha yao, huku akilitaka Bunge kujadili na kutoa maoni kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2027/28.

TAFUTA HABARI
Kamusi
Social Plugin