Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TBS YATOA ELIMU YA VIWANGO VYA UBORA KWA WAJASIRIAMALI ZAIDI YA 600 KATIKA MAONESHO YA SIDO KITAIFA KAHAMA




Na Shaban Njia, KAHAMA.


SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeshiriki Maonesho ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kwa lengo la kutoa elimu kwa wajasiriamali na wasindikaji wa bidhaa kuhusu taratibu za kupata alama za ubora wa bidhaa, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kuongeza ushindani na kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.


Elimu hiyo inalenga kuwajengea uwezo wajasiriamali kutambua umuhimu wa kuzingatia viwango vya ubora katika uzalishaji wa bidhaa, hatua inayoweza kuongeza imani ya watumiaji na kufungua fursa za kibiashara katika masoko mbalimbali.



Aidha, maonyesho hayo yameanza rasmi Oktoba 21 yakifunguliwa na Waziri wa Viwanda, Mheshimiwa Judith Kapinga na kushirikisha zaidi ya wajasiriamali 600 kutoka maeneo mbalimbali nchini.


Kadhalika, maonyesho hayo yamewapa wajasiriamali fursa ya kukutana na taasisi mbalimbali, ikiwemo TBS ili kupata elimu, huduma na taarifa zinazoweza kuwasaidia kuboresha bidhaa zao na kuendeleza biashara zao katika masoko ya ndani na nje.


Akizungumza na vyombo vya habari lro katika banda la maonyesho lililopo viwanja vya Magufuli, Ofisa Masoko Mwandamizi wa TBS, Denis Mzamilu amesema hadi sasa wajasiriamali 45 kutoka mabanda mbalimbali wamefikiwa na kupewa elimu kuhusu viwango vya ubora katika uzalishaji wa bidhaa.


Amesema, bidhaa ambazo hukidhi viwango vya ubora hupewa Nembo ya TBS ambayo kwa kiasi kikubwa huwezesha bidhaa zao kuongeza tija sokoni  na hivyo kuweza kuuzwa katika masoko ya ndani, kitaifa na kikanda kwa urahisi zaidi.


Hata hivyo Denisi amesema alama za TBS inalenga kuwawezesha wajasiriamali wadogo kuboresha ubora wa bidhaa zao na kuongeza fursa za kibiashara kupitia uthibitisho wa viwango vinavyotambulika hatua itakayofanya kuwa na ushindani mkubwa sokoni.


Pia ametoa wito kwa wajasiriamali kutembelea banda la TBS lililopo karibu na banda SIDO katika lango la kuingilia ndani ya uwanja wa maonyesho na kupata elimu, utaratibu wa alama za ubora wa bidhaa na watahudumiwa na maofisa waliopo muda wote wa maonyesho.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com