Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPENI YA ‘ONGEA NA KAMANDA’ YAFIKA MHUNZE, POLISI KISHAPU WATOA ELIMU YA UKATILI NA USALAMA KANISANI

 

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu , Inspector Rose R. Mbwambo, akitoa elimu kwa waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Yohane Maria Vianney, Mhunze, kuhusu mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ulinzi wa watoto na umuhimu wa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kupitia kampeni ya “Ongea na Kamanda” ya Jeshi la Polisi.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu , Inspector Rose R. Mbwambo, akitoa elimu kwa waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Yohane Maria Vianney, Mhunze, kuhusu mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ulinzi wa watoto na umuhimu wa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kupitia kampeni ya “Ongea na Kamanda” ya Jeshi la Polisi.
Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kishapu, SP Chacha M. Mwita, akitoa elimu kwa waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Yohane Maria Vianney, Mhunze, kuhusu ulinzi na usalama, mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kusalimisha silaha haramu kupitia kampeni ya “Ongea na Kamanda” ya Jeshi la Polisi.
Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu, SSGT. Grace Cyprian, akitoa elimu kwa waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Yohane Maria Vianney, Mhunze, kuhusu aina mbalimbali za ukatili wa kijinsia, ulinzi wa watoto na umuhimu wa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili ili kuhakikisha waathirika wanapata ulinzi na msaada unaostahili.
Baba Paroko wa Parokia ya Mt. Yohane Maria Vianney, Mhunze, Padre Josephat Mahalu, akizungumza kuhusu umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi wa dini, wananchi na Jeshi la Polisi katika kupinga ukatili wa kijinsia, kuimarisha ulinzi na usalama na kudumisha amani katika jamii.

Na Sumai Salum-Kishapu

Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mt. Yohane Maria Vianney, Mhunze, Jimbo Katoliki la Shinyanga, wamepatiwa elimu kuhusu mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ulinzi na usalama wa raia, kudumisha amani pamoja na umuhimu wa kusalimisha silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria kupitia kampeni ya “Ongea na Kamanda” ya Jeshi la Polisi.

Akitoa elimu hiyo kupitia Misa Takatifu iliyofanyika Jumapili, Oktoba 25, 2026, iliyoongozwa na Baba Paroko wa parokia hiyo, Padre Josephat Mahalu, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kishapu, SSP Chacha M. Mwita, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi katika kuimarisha amani na usalama, huku akiwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa mamlaka husika kabla ya Oktoba 31, 2026.

Chacha amesema wananchi wanapaswa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na kutoficha wahalifu wala silaha haramu, akionya kuwa muda wa kusalimisha silaha hizo utakapokamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kumiliki silaha hizo kinyume cha sheria.

“Amani na usalama vinaanza na kila mmoja wetu. Wananchi wanapaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na kuhakikisha hawafichi wahalifu wala silaha haramu. Tunatoa wito kwa wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha kwa mamlaka husika kabla ya Oktoba 31, 2026. Baada ya tarehe hiyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria,” amesema Chacha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu, INSP. ROSE R. MBWAMBO, amewataka waumini na wananchi kwa ujumla kutokukubali vitendo vya ukatili wa kijinsia kuendelea katika jamii, akisisitiza kuwa kila mtu ana wajibu wa kulinda haki, utu na usalama wa wengine.
Mbwambo amewahimiza wazazi, walezi na viongozi wa jamii kutoa taarifa za vitendo vya ukatili badala ya kuvificha kwa misingi ya undugu, urafiki au kulinda heshima ya familia, ili wahusika wawajibishwe kwa mujibu wa sheria.

“Ukatili wa kijinsia haupaswi kufumbiwa macho wala kufichwa kwa sababu ya undugu, urafiki au kulinda heshima ya familia. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kukemea vitendo hivyo, kutoa taarifa kwa mamlaka husika na kuhakikisha wanawake, watoto na watu wengine walio katika mazingira hatarishi wanalindwa dhidi ya ukatili. Jamii inapaswa kuwa sehemu ya kutafuta suluhisho, si sehemu ya kuficha uhalifu,” amesema Mbwambo.

Naye Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Kishapu, SSGT Grace Cyprian, amesisitiza umuhimu wa jamii kutambua aina mbalimbali za ukatili, ikiwemo ukatili dhidi ya wanawake na watoto, na kuchukua hatua za mapema kuzuia madhara.

Amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama, huku akihimiza wananchi kutowalaumu au kuwanyamazisha waathirika wa ukatili, bali kuwasaidia kupata ulinzi na huduma zinazostahili na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
“Watoto na waathirika wa ukatili wanahitaji ulinzi, msaada na mazingira salama, si kulaumiwa au kunyamazishwa. Tunawaomba wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kuwa macho dhidi ya viashiria vya ukatili na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika. Kila mmoja ana nafasi ya kuzuia ukatili kwa kuzungumza, kutoa taarifa na kuhakikisha waathirika wanapata msaada unaostahili,” amesema Grace.

Kwa upande wake, Baba Paroko wa Parokia ya Mt. Yohane Maria Vianney, Mhunze, Padre Josephat Mahalu, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuwafikia wananchi kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo nyumba za ibada, kwa lengo la kutoa elimu ya ulinzi na usalama, kupinga ukatili na kuimarisha amani.

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza uelewa wa jamii na kujenga uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, huku akihimiza elimu hiyo iendelee kutolewa ili watu wafahamu wajibu wao katika kuzuia uhalifu na kulinda haki za wengine.

“Ninalipongeza Jeshi la Polisi kwa kuwafikia wananchi kupitia majukwaa mbalimbali, ikiwemo nyumba za ibada, ili kutoa elimu ya ulinzi na usalama. Hii ni hatua muhimu kwa sababu usalama wa jamii hauwezi kujengwa na Jeshi la Polisi pekee bila ushirikiano wa wananchi. Tunawaomba waumini na jamii kwa ujumla kuzingatia elimu inayotolewa, kufuata sheria na kushirikiana na vyombo vya usalama katika kupinga ukatili na kudumisha amani,” amesema Padre Mahalu.

Kampeni ya “Ongea na Kamanda” ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano na wananchi katika kudumisha amani na usalama. Kupitia kampeni hiyo, wananchi wanahimizwa kutoa taarifa za uhalifu, kuzuia ukatili, kulinda watoto na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi pamoja na kushirikiana na vyombo vya dola kubaini viashiria vya vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha na mali.

Jeshi la Polisi linaendelea kuhimiza wananchi kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuzingatia sheria, kutoa taarifa kwa wakati na kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha Wilaya ya Kishapu inaendelea kuwa eneo lenye amani, usalama na utulivu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com