Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE CHEREHANI AWATAKA WATUMISHI KUBANA MATUMIZI YA FEDHA ZA MIRADI


Na Steve Kanyefu - Ushetu

Mbunge wa Jimbo la Ushetu mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani, amewataka wasimamizi wa miradi ya wananchi kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali, wananchi pamoja na wadau mbalimbali zinasimamiwa ipasavyo ili ziweze kukamilisha miradi iliyokusudiwa kwa kiwango kinachostahili.

Cherehani ametoa kauli hiyo leo Oktoba 7,2026  baada ya kukagua na kuzindua Zahanati ya Kijiji cha Nyawishi, Kata ya Chambo, ambapo amesema hajaridhishwa na namna fedha zilizotumika katika ujenzi wa zahanati hiyo zilivyosimamiwa.

Amesema wasimamizi wa miradi wanapaswa kubana matumizi na kuhakikisha fedha zinatumika kwa vipaumbele vya msingi ili kukamilisha mahitaji yote ya mradi husika.

“Nikuombe DMO angalieni namna ya kubana matumizi, hizo milioni 60 zikamilishe hatua ya ujenzi ikiwa ni pamoja na kuweka madirisha ya vioo, gharama yake haizidi milioni tatu. Baneni matumizi, fedha zikamilishe miradi,” amesema.

Cherehani amesisitiza kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinapaswa kusimamiwa kwa umakini na kutumika kwa kuzingatia mahitaji halisi ya mradi, ili kuhakikisha wananchi wanapata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali, wananchi na wadau mbalimbali.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa Zahanati ya Nyawishi, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Mathias Saninga, amesema ujenzi ulianza mwaka 2009 kwa nguvu za wananchi ambao walifanikiwa kukamilisha boma la jengo hilo.

Saninga amesema hadi sasa Serikali imeshatoa zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.

“Zahanati ilipokea kiasi cha shilingi milioni 50 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na mwezi Machi 2026 kiasi cha shilingi milioni 60 kiliingizwa katika akaunti ya Kijiji cha Chambo,” amesema.

Katika taarifa hiyo, Mganga Mfawidhi pia ameainisha changamoto zinazoikabili zahanati hiyo kuwa ni pamoja na upungufu wa watumishi wa afya, ukosefu wa maji na ukosefu wa nyumba za watumishi.

Amesema mpaka sasa ujenzi wa zahanati hiyo umefikia asilimia 60 na ikikamilika inatarajiwa kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 4,270 wa Kijiji cha Nyawishi pamoja na maeneo ya jirani.























Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com