Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CEO MALULA TV AKUTANA NA KATIBU WA CCM SHINYANGA KUJADILI TAMASHA KUBWA LA GOSPEL


Mkurugenzi Mtendaji (CEO) wa Malula TV, Daniesa Malula, amekutana na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Bi. Sofia Kibaba, kwa mazungumzo kuhusu maandalizi ya tamasha kubwa la muziki wa Injili linalotarajiwa kufanyika mkoani humo.

Katika mazungumzo hayo, wamejadili umuhimu wa tamasha hilo katika kuwaunganisha waimbaji wa nyimbo za Injili, kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha huduma ya uinjilisti kupitia muziki wa Gospel.

Tamasha hilo limebeba malengo matano muhimu, yakiwemo kuwaunganisha waimbaji wa nyimbo za Injili mkoani Shinyanga, kufanya Live Recording, kuzindua rasmi EP yenye nyimbo 20, pamoja na kuadhimisha miaka 20 ya huduma ya Shinyanga Amazing Gospel katika kueneza Injili kupitia muziki.

Akizungumza katika mazungumzo hayo, Bi. Sofia Kibaba ameeleza kufurahishwa kwake na juhudi zinazofanywa na waandaaji wa tamasha hilo, huku akimpongeza Daniesa Malula kwa ubunifu wake na dhamira ya kuwakutanisha vijana pamoja na waimbaji wa Gospel kwenye jukwaa moja.

Aidha, ameupongeza mpango wa kampeni ya “Kijana Smart Yuko Ndani ya Yesu,” inayolenga kuwahamasisha vijana kumweka Mungu mbele katika maisha yao na kutumia vipaji walivyopewa kwa ajili ya kujenga jamii yenye maadili mema.

Bi. Kibaba amewatakia waandaaji mafanikio katika maandalizi ya tamasha hilo, huku akiahidi kushiriki na kutoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi ili kuunga mkono tukio hilo la kiroho na kimuziki.

Tamasha hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha umoja miongoni mwa waimbaji wa Gospel, kukuza vipaji vya vijana na kuendeleza huduma ya uimbaji wa Injili mkoani Shinyanga, sambamba na kuhamasisha vijana kutumia vipaji vyao katika shughuli zenye manufaa kwa jamii.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com