Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), Yohana Goshashy akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule za Msingi kuhusu aina ya nyoka na sumu katika kuadhimisha Wiki ya Kuzuia Kung’atwa na Nyoka Kitaifa iliyofanyika Kibaha mkoani Pwani, Septemba 22, 2026.
*****************
Na Okello Thomas
Katika kuadhimisha Wiki ya Kuzuia Kung’atwa na Nyoka Kitaifa, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu(NPCC), imetoa elimu kuhusu sumu ya nyoka na namna ya kujikinga na madhara yatokanayo na kung’atwa na nyoka kwa wanafunzi na walimu wa shule za msingi zilizopo Kibaha mkoani Pwani, Septemba 22, 2026.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu hiyo, Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Yohana Goshashy amesema utoaji wa elimu kwa wanafunzi ni sehemu ya jitihada za Mamlaka kuongeza uelewa wa jamii kuhusu sumu na namna ya kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matukio ya sumu, ikiwemo kung’atwa na nyoka.
“Dhumuni la kutoa elimu hii kwa wanafunzi ni kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu nyoka wenye sumu, namna ya kujikinga na kung’atwa pamoja na hatua sahihi za kuchukua endapo tukio hilo litatokea. Tunataka wanafunzi wajue kwamba kung’atwa na nyoka ni tukio linalohitaji hatua za haraka na sahihi za kitabibu, hivyo ni muhimu kumfikisha mgonjwa kwenye kituo cha afya mapema,” alisema Goshashy.
Amesema wanafunzi ni kundi muhimu katika jamii kwa kuwa elimu wanayoipata shuleni inaweza kuwasaidia kujilinda wao wenyewe, kuwasaidia wenzao na pia kufikisha ujumbe huo kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.
Aidha, ameongeza kuwa baadhi ya imani na taratibu zisizo sahihi zinazofanywa na jamii baada ya mtu kung’atwa na nyoka zinaweza kuongeza madhara kwa mgonjwa, hivyo ni muhimu jamii kupata elimu sahihi kutoka kwa wataalamu.
“Tunasisitiza jamii kuacha kutumia njia zisizo salama katika kumhudumia mtualiyeng’atwa na nyoka. Mtu aliyeng’atwa anapaswa kupata huduma ya kitabibu haraka iwezekanavyo. Elimu hii tunayoitoa shuleni inalenga pia kuwafanya wanafunzi wawe mabalozi wa ujumbe huu katika familia zao na kwenye jamii,” alisisitiza Goshashy.
Kwa upande wake, Mwalimu anayesimamia masuala ya Afya katika Shule ya Msingi Kanesa iliyopo Kibaha mkoani Pwani, Fatuma Nkya ameeleza kuwa elimu hiyo imekuwa na faida kubwa kwa wanafunzi na walimu kwa sababu imewaongezea uelewa kuhusu namna ya kutambua hatari zinazohusiana na nyoka pamoja na hatua za kuchukua pale tukio la kung’atwa linapotokea.
Amesema kabla ya elimu hiyo, baadhi yawanafunzi na hata watu katika jamii wanaweza kuwa na taarifa zisizo sahihi kuhusu namna ya kumsaidia mtu aliyeng’atwa na nyoka, jambo ambalo linaweza kuchelewesha upatikanaji wa matibabu.
“Elimu hii imekuwa muhimu sana kwetu kwa sababu imewasaidia wanafunzi na walimu kufahamu mambo ambayo awali hatukuwa na uelewa wa kutosha. Sasa tunajua umuhimu wa kuchukua hatua kwa haraka na kumpeleka mhanga kwenye kituo cha afyabadala ya kutumia njia ambazo hazijathibitishwa kitaalamu,” alisema Nkya.
Alisema wanaishukuru Mamlaka kwa kufikishia elimu hiyo. Na wanawaona wanafunzi kama sehemu muhimu ya kusambaza elimu hii kwa sababu wanapofundishwa jambo muhimu, wanaweza kwenda kuwaeleza wazazi, ndugu na marafiki. Hivyo, elimu hiyohaibaki shuleni pekee, bali inakwenda hadi kwenye jamii.
Naye mmoja wa wanafunzi walioshiriki katika mafunzo hayo kutoka Shule ya Msingi Kanesa, Samir Kadili ameipongeza Mamlaka kwa kuwafikishia elimu hiyo, akisema imewasaidia kufahamu namna ya kujikinga na nyoka na nini cha kufanya endapo mtuatang’atwa.
“Tunawashukuru Mamlaka kwa kutupatia elimu hii kwa sababu tumefahamu mambo ambayo hatukuyajua. Tumejifunza kuwa tunapaswa kuwa makini tunapokuwa maeneo ambayo kuna uwezekano wa kuwepo kwa nyoka na pia tumeelewa umuhimu wakumpeleka haraka hospitalini mtu aliyeng’atwa,” alisema Kadili.
Elimu hiyo ni sehemu ya shughuli za Wiki ya Kuzuia Kung’atwa na Nyoka Kitaifa,ambayo inalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kuzuia matukio yakung’atwa na nyoka, kutambua hatari zinazohusiana na sumu ya nyoka na kuchukua hatua sahihi pindi tukio linapotokea.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Kanesa, Fatuma Nkya (kulia) akimkaribisha Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu (NPCC), Yohana Goshashy(kushoto)alipowasili na wataalam kutoka Mamlaka kutoa elimu ya sumu kwa wanafunzi wa shule hiyo iliyopo Kibaha, Pwani.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kanesa wakifuatilia elimu ya kujikinga dhidi ya sumu ya nyoka yaliyowasilishwa na wataalam kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (hawapo pichani).

Wanafunzi wakiuliza maswali kwa mwezeshaji (hayupo pichani), kuhusu kujikinga na hatua za kuchukua dhidi ya matukio ya nyoka na sumu zake.
Wanafunzi wakiandika maelezo kuhusu namna ya kujikinga na matukio ya sumu wakati wakipewa elimu ya sumu na wataalam kutoka Mamlaka.
Mtumishi wa Mamlaka, Amina Omary, akiandika maswali yaliyoulizwa na wanafunzi katika kuadhimisha Wiki ya Kuzuia Kung’atwa na Nyoka Kitaifa iliyofanyika Kibaha mkoani Pwani, Septemba 22, 2026.
Watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wakizungumza na wanafunzi wakati wa utambulisho kabla utoaji elimu ya kujikinga na mtukio ya sumu kwa wanafunzi wa shule za msingi zilizopo Kibaha, Pwani.
Mtumishi wa Mamlaka, Christer Mwageni (katikati) akizungumza na mwalimu wa Shule ya Msingi Boko Timiza (kushoto) wakati wa utoaji elimu kuhusu kujikinga na matukio ya sumu ya nyoka yaliyofanyika Kibaha, Pwani.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kanesa, Samir Kadili, akitoa neno la shukrani kwa wawezeshaji kutoka Mamlaka baada ya kukamilisha utoaji wa elimu.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com
Social Plugin