Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

EACOP KUANZA KUSAFIRISHA MAFUTA GHAFI JANUARI 15, 2027


Na Mbuke Shilagi - Kagera.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unatarajiwa kuanza rasmi kusafirisha mafuta ghafi ifikapo Januari 15, 2027, huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa umefikia asilimia 87.7.

Hayo yameelezwa na Jumanne Mohamed Saidi, Mratibu wa Utekelezaji wa Mradi wa EACOP kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), wakati akizungumza na waandishi wa habari wa Mkoa wa Kagera katika warsha iliyofanyika ELCT Hotel, Manispaa ya Bukoba.

Saidi amesema mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi kwa siku na unatarajiwa kufanya kazi kwa kipindi cha miaka 25.

Amesema hadi sasa mradi huo umelipa jumla ya shilingi bilioni 35.6 kama fidia kwa wananchi 10,144 kati ya 10,223 waliostahili kulipwa, sawa na asilimia 99.5 ya wananchi wote walioguswa na zoezi la fidia.

Aidha, amesema mradi umejenga jumla ya nyumba 340 za kisasa kwa wananchi 294 walioguswa moja kwa moja na ujenzi wa bomba hilo.

Kwa Mkoa wa Kagera pekee, jumla ya nyumba 119 zimejengwa kwa wananchi 118 katika wilaya za Misenyi, Bukoba, Muleba na Biharamulo. Kati ya nyumba hizo, nyumba 25 zimejengwa Misenyi, 21 Bukoba, 71 Muleba na nyumba mbili Biharamulo.

Mradi wa EACOP unaanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Chongoleani mkoani Tanga, Tanzania, ukiwa na urefu wa jumla ya kilomita 1,443. Kati ya urefu huo, kilomita 1,147 zipo Tanzania na kilomita 296 zipo nchini Uganda.

Mradi huo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi katika Bandari ya Chongoleani kwa ajili ya kusafirishwa kwenda katika masoko ya kimataifa, huku ukitarajiwa kuanza rasmi shughuli zake Januari 15, 2027.

Akizungumzia masuala ya nishati katika warsha hiyo, Marie Msellem, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, amesema kuwa gesi asilia tayari inatumika na wananchi katika baadhi ya maeneo nchini, ikiwemo Mtwara, Lindi na Dar es Salaam.

Msellem amesema pamoja na uwepo wa matumizi ya gesi asilia katika maeneo hayo, bado wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya nishati hiyo, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili wananchi waweze kuelewa matumizi sahihi na salama ya gesi asilia pamoja na fursa na manufaa yanayopatikana kutokana na rasilimali hiyo.

Amesisitiza kuwa waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu sekta ya mafuta na gesi, ikiwemo matumizi ya gesi asilia na fursa zinazotokana na rasilimali hizo.



















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com