Na Mwandishi Wetu
Geneva, Uswisi, Julai 09, 2026– Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.) amepokea Tuzo ya Kimataifa ya WSIS Prizes 2026 kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
Tuzo hiyo imetolewa kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano, ambao umeongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na maeneo ambayo awali hayakuwa na huduma nchini.
Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo imefanyika Geneva, Uswisi, na ni utambuzi wa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini.
Akizungumza baada ya kuipokea tuzo hiyo, Waziri Kairuki amesema mafanikio hayo ni matokeo ya dhamira ya Rais Samia ya kuhakikisha kila raia anapata huduma za mawasiliano bila kujali eneo alilopo.
“Serikali imedhamiria kufunga pengo la kidijitali. Minara 758 imetoa fursa kwa wananchi wetu wa vijijini kupata mawasiliano, huduma za kibenki, elimu na afya kidijitali,” alisema Waziri Kairuki.
Mradi wa minara 758 ulizinduliwa rasmi na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 10 Aprili, 2026.
Mbali na tuzo hiyo, Tanzania ilipata uteuzi katika vipengele saba (7) vya Tuzo za WSIS 2026 na kuibuka na tuzo mbili kwa ujumla. Pia imetunukiwa vyeti vya kutambua miradi mingine iliyofanya vizuri.
Tuzo za WSIS hutolewa kila mwaka na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano ITU kutambua miradi bora duniani inayochangia katika kukuza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.


Social Plugin