Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa wa pili kutoka kulia akiwa pamoja na mwenyeji wake mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed baada ya kuzindua jengo la mapumziko ya muda mfupi kwa abiria katika uwanja wa ndege wa Songea unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa kusini Na Regina Ndumbaro
Songea-Ruvuma
Uwekezaji wa Serikali wa shilingi milioni 842 katika upanuzi wa jengo la mapumziko ya muda mfupi kwa abiria katika uwanja wa ndege wa Songea unatarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa biashara, uwekezaji na utalii, baada ya kuongeza uwezo wa uwanja huo kuhudumia abiria 300 kwa wakati mmoja.
Akizungumza baada ya kuwasili uwanja huo wa ndege wa Songea Waziri wa Uchukuzi mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa, amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kukidhi ongezeko la wasafiri, ambapo pamoja na jengo hilo, maboresho mengine yamehusisha ukarabati wa njia ya kurukia na kutua ndege, upanuzi wa maegesho ya ndege, ufungaji wa taa za kuongozea ndege na vifaa vya kisasa vya mawasiliano.
Amesema hatua hiyo itaenda sambamba na mpango wa kuongeza safari za ndege kati ya Dar es Salaam na Songea.
Amesema kuimarika kwa huduma za usafiri wa anga kutarahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kuongeza fursa za kiuchumi na kuifanya Ruvuma kuvutia zaidi wawekezaji na watalii.
Aidha, amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa ufanisi.
Akizungumza katika hafla hiyo, mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema Serikali pia imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 0.8 kuelekea uwanjani.
Naye mhandisi Focus Kadege amesema mradi huo umekamilika kwa mafanikio na uko tayari kuboresha huduma za usafiri wa anga, ukiwa sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha miundombinu na kukuza uchumi wa mkoa wa Ruvuma.




Social Plugin