Na Mwandishi Wetu
WANAFUNZI wanaosoma mkondo wa elimu ya amali katika Shule ya Sekondari Dar es Salaam wameeleza kuwa ufadhili wa vifaa vya ushonaji uliotolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) umeleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa mafunzo ya vitendo, hatua inayowajengea uwezo wa kujiajiri na kuanzisha biashara mara baada ya kuhitimu masomo yao.
Akizungumza leo Julai 8, 2026 katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mwanafunzi wa kidato cha tatu anayesoma fani ya ushonaji, Mariam Mitimingi, amesema alichagua mkondo wa amali baada ya kuona unatoa fursa kubwa za ajira na kujiajiri tofauti na kutegemea ajira rasmi pekee.
Amesema kupitia mafunzo hayo, wanafunzi wanapata ujuzi wa kubuni na kushona mavazi mbalimbali huku wakiwa bado shuleni, jambo linalowawezesha kujijengea msingi imara wa taaluma na biashara za baadaye.
"Nilichagua fani ya ushonaji kwa sababu niliona inanipa ujuzi wa moja kwa moja. Nikimaliza kidato cha nne nitakuwa tayari kuanzisha shughuli yangu, kufungua kiwanda cha ushonaji au hata kituo cha kutoa mafunzo kwa wengine. Tayari tukiwa kidato cha tatu tuna uwezo wa kubuni na kushona mavazi mbalimbali ya kiafrika kutokana na mafunzo tunayopata," amesema Mariam.
Ameeleza kuwa kabla ya shule yao kupokea mashine na vifaa kutoka TEA, walilazimika kwenda katika Chuo cha VETA Chang'ombe kupata mafunzo ya vitendo, hali iliyowafanya kupoteza muda mwingi pamoja na kukosa baadhi ya vipindi vya masomo darasani.
"Kwa sasa tunafanya mafunzo yote hapa shuleni. Ratiba imekuwa nzuri zaidi kwa sababu tunasoma masomo ya darasani na wakati huo huo tunapata mafunzo ya vitendo bila kulazimika kusafiri. Tunashukuru sana TEA kwa kutupatia vifaa hivi," amesema.
Nae Emiliano Shauri ambaye anasoma mkondo wa elimu ya amali katika fani ya ushonaji wa shule hiyo, amesema mbali na kupata maarifa ya darasani, mafunzo ya ushonaji yanamwezesha kushona mavazi mbalimbali kwa wateja na kujipatia kipato hata kabla ya kuendelea na masomo ya juu.
"Nimechagua fani ya ushonaji kwa sababu inanipa ujuzi ambao unaweza kunisaidia kujiajiri. Baada ya kumaliza kidato cha nne ninaweza kufungua biashara yangu ya ushonaji huku nikisubiri kuendelea na masomo. Malengo yangu ni kusoma masomo ya ubunifu wa mavazi na teknolojia ya nguo ili siku zijazo niwe mbunifu mkubwa na kuona bidhaa zangu zikitengenezwa viwandani," amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Dar es Salaam, Mwalimu Semi Njau, amesema ufadhili wa mashine za ushonaji kutoka TEA umeboresha kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa mkondo wa elimu ya amali shuleni hapo.
Amesema vifaa hivyo vimewawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo badala ya kutegemea nadharia pekee, jambo linalowajengea stadi muhimu za kazi zitakazowasaidia kujiajiri, kuajiriwa na hata kuwaajiri wengine baada ya kuhitimu.
"Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa kuwa sehemu ya kutimiza ndoto za vijana wetu. Leo hii wanafunzi hawamalizi elimu ya sekondari wakiwa na maarifa ya nadharia pekee, bali wanahitimu wakiwa na ujuzi unaowawezesha kujitegemea kiuchumi," amesema.
Mwalimu Njau amesema mwanzoni baadhi ya wazazi walikuwa hawajaelewa dhamira ya Serikali ya kuanzisha mkondo wa elimu ya amali, lakini hali imebadilika baada ya kuona matokeo ya wanafunzi pamoja na ufadhili uliofanywa na TEA.
Ameeleza kuwa wazazi sasa wanaunga mkono programu hiyo kwa kuona mashine na vifaa vinavyotumika na wanafunzi kujifunza kwa vitendo, jambo linalowapa imani kuwa watoto wao wanapata elimu yenye tija inayowaandaa kwa soko la ajira na kujiajiri.
Mkondo wa elimu ya amali unaendelea kuwa sehemu ya maboresho ya mfumo wa elimu nchini kwa lengo la kuwajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo, ubunifu na uwezo wa kujitegemea mara wanapomaliza masomo yao.
Rozana Magubika mwalimu wa mkondo wa elimu ya amali katika Shule ya Sekondari Dar es Salaam amesema shule hiyo ilianza kutekeleza mkondo wa elimu ya amali mwaka 2024 na kwa sasa ina wanafunzi 63 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu wanaosomea fani ya ubunifu wa mavazi na teknolojia ya ushonaji.
Amesema kupitia ufadhili wa TEA, shule imepokea mashine 17 za kisasa za ushonaji zenye matumizi mbalimbali, zikiwemo mashine za kushona nguo, mashine za kumalizia kazi (overlock), mashine za kutengeneza vifungo, mashine za urembo wa nguo pamoja na mashine za chain stitch zinazotumika kutengeneza nakshi na mapambo ya mavazi.
Aidha, shule imepokea mashine ya kisasa ya kukatia vitambaa pamoja na vifaa vingine vya kufundishia vinavyorahisisha mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi. Thamani ya vifaa hivyo ni zaidi ya shilingi milioni 44.
Mamlaka ya Elimu Tanzania inaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali wa elimu ikiwamo mashirika ya Umma, mashirika binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi mbalimbali na watu binafsi kuchangia maendeleo ya elimu kwa kuchangia rasilimali fedha na vifaa katika Mfuko wa Elimu wa Taifa ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia kote nchini.









Social Plugin