Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MHITA APONGEZA KISHAPU KUPATA HATI SAFI ATOA MAELEKEZO MAPYA


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wilayani Kishapu mkoani humo cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika Julai 10,2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Na Sumai Salum-Kishapu


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kupata hati safi ya ukaguzi kwa miaka mitano mfululizo, akisema mafanikio hayo ni ushahidi wa usimamizi mzuri wa fedha za umma na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali.


Akizungumza katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika Julai 10,2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo, Mhe. Mhita amesema Halmashauri hiyo ina jumla ya hoja 108 za ukaguzi, ambapo hoja 23 zimefungwa huku hoja 80 zikiwa bado katika hatua mbalimbali za utekelezaji.


Amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha hoja zilizobaki zinashughulikiwa kwa haraka ili kuongeza uwajibikaji na kuendelea kulinda hadhi ya halmashauri hiyo. "Mmefanya vizuri kwa kuendelea kupata hati safi, lakini ni muhimu kuhakikisha hoja zilizobaki zinatekelezwa kwa wakati ili kuimarisha zaidi usimamizi wa fedha za umma,".


Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Mkurugenzi Mtendaji, Baraza la Madiwani na Menejimenti katika kutekeleza maelekezo ya Serikali na kutafsiri maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Aidha, Mhita amehimiza Halmashauri kuendelea kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kubuni na kuibua vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuboresha vilivyopo. "Pamoja na kufanya vizuri, ni lazima muongeze mapato ya ndani kwa kutumia fursa na vivutio vilivyopo Kishapu,. Hata hivyo, hatua hizo zisiwe za kuwaongezea wananchi mzigo wa kodi, bali ziende sambamba na utoaji wa elimu ya kodi na kuboresha mazingira ya biashara," ameongeza.


Ametolea mfano Mnada wa Mhunze, akisema unapaswa kuboreshwa kwa kuweka miundombinu rafiki na ya kisasa ili kuvutia wafanyabiashara na kuongeza mapato ya Serikali na Halmashauri huku akiwataka Halmashauri kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha wote wanaokwepa kulipa kodi wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.


Mkuu huyo wa Mkoa amesema tangia kuanza kwa awamu ya pili ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Shinyanga umepokea zaidi ya shilingi trilioni 1.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na maji.

Amesisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kusimamiwa kwa umakini ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha,."Niwaombe, muwe kama mimi nisivyo 'ndumila kuwili', tusisite kulinda rasilimali zetu. Waheshimiwa madiwani mnapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora na thamani ya fedha inaonekana," amesisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita akisisitiza jambo kwenye kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wilayani Kishapu mkoani humo cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika Julai 10,2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo


Mkuu huyo wa Mkoa pia amezungumzia umuhimu wa kuendeleza umoja na ushirikiano kati ya Mkuu wa Wilaya, Madiwani, Mkurugenzi na Menejimenti yake katika utekelezaji wa bajeti zinazogusa makundi maalumu, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.


Aidha, ametoa wito kwa watumishi na viongozi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kuhifadhi nyaraka zote za manunuzi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu ili kuepusha hati zenye mashaka siku zijazo.


Kwa upande wake, Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, George Silumbwe, aliyesoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Emmanuel Johnson, amesema Halmashauri ilikuwa na hoja 56 za ukaguzi za miaka ya fedha 2016/2017 hadi 2023/2024 ambazo hazikuwa zimefungwa.


Amesema baada ya uhakiki, hoja 18 zilifungwa huku hoja 38 zikiendelea kufanyiwa kazi. Aidha, katika taarifa ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ilikuwa na hoja 32, ambapo baada ya majibu ya Menejimenti na uhakiki wa Mkaguzi wa Nje wa Mkoa wa Shinyanga, hoja tano zilifungwa na hoja 27 zimeendelea kuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.


Silumbwe pia amewasilisha taarifa za utekelezaji wa mapendekezo ya CAG katika Mfuko wa Pamoja wa Afya (HBF) pamoja na Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu (WYDF).

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe Josephat Limbe akizungumza katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wilayani Kishapu mkoani humo cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika Julai 10,2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mhe. Josephati Limbe, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo aliyoyatoa na kuahidi kuwa Baraza la Madiwani kwa kushirikiana na Mkurugenzi na Menejimenti watayafanyia kazi ili kuendelea kuimarisha utendaji wa halmashauri hiyo.



Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu imeendelea kuweka rekodi ya kupata hati safi ya ukaguzi kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hadi 2024/2025, hatua inayodhihirisha kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma na uwajibikaji.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Peter Masindi akizungumza katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wilayani Kishapu mkoani humo cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika Julai 10,2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson akizungumza katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wilayani Kishapu mkoani humo cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika Julai 10,2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Mweka Hazina wa Halmashauri ya wilaya Kishapu mkoani Shinyanga George Silumbwe akisoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Emmanuel Johnson kwenye kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani wilayani humo cha kujadili taarifa hiyo kilichofanyika Julai 10,2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo
Makamo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Mhe. Enock Reuben akifuatilia kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani humo cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika Julai 10,2026 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo









































































Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com