Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSIGWA ATOA MWELEKEO WA SERIKALI: AFYA, FURSA ZA VIJANA NA ULINZI WA AMANI VYAPEWA KIPAUMBELE



NA DOTTO KWILASA,DODOMA

Serikali imeeleza hatua mbalimbali inazochukua katika kuimarisha huduma za afya, kukuza fursa za kiuchumi kwa vijana na kulinda amani na usalama wa nchi, ikisisitiza kuwa maendeleo ya Taifa hayawezi kupatikana bila mazingira salama na wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kupitia uwekezaji katika sekta za afya, biashara na huduma mbalimbali za kijamii, huku akiwataka vijana kutumia fursa zilizopo badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Soko la Machinga na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo Julai 22,2026 jijini Dodoma, Msigwa amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya kupitia fedha za maendeleo zinazotekelezwa na TAMISEMI, hatua iliyosaidia kuongeza miundombinu na huduma kwa wananchi.

Amesema Serikali imejenga majengo 87 ya huduma za dharura, majengo 30 ya ICU, vituo viwili vya magonjwa ya milipuko, mitambo 21 ya kuzalisha hewa tiba, nyumba 432 za watumishi wa afya pamoja na magari 382 ya wagonjwa.

Kwa mujibu wake, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka tangu mwaka 2021, ambapo zahanati zimeongezeka kutoka zaidi ya 7,000 hadi zaidi ya 8,000, huku hospitali zikiongezeka kutoka 444 hadi 475.

Amesema Serikali pia imeimarisha upatikanaji wa dawa kupitia MSD kwa gharama ya shilingi bilioni 242.7, na kiwango cha upatikanaji wa dawa kufikia asilimia 88.8.

Akizungumzia fursa za uchumi Kwa vijana amesema,Msigwa amesema Serikali imeendelea kufungua fursa kwa vijana kupitia mikopo, ruzuku, mafunzo na ujenzi wa masoko, akiwataka kuacha kupoteza muda katika vurugu na badala yake wajikite katika shughuli za maendeleo.

"Kijana huna sababu ya kulalamika. Fanya biashara, lima au fuga,acheni kupoteza muda kuhamasishana kufanya vurugu,hakuna nchi yoyote iliyoendelea kwa watu kukaa bila kufanya kazi," amesema.

Amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwa biashara, kilimo na ufugaji ili kuwawezesha wananchi kujiajiri na kuongeza kipato.

Akizungumzia Soko la Machinga Msigwa amesema ameridhishwa na maendeleo yake baada ya kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wafanyabiashara wa ndani, huku akieleza kuwa Serikali inaendelea kujenga masoko mapya ikiwemo Kizota na Kisasa pamoja na maeneo mengine nchini.

Pia amesema Serikali inaendelea kupeleka fedha katika miradi ya maendeleo kila mkoa na kuwataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji zinazosambazwa mitandaoni kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com