Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Msalala kilichojadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Picha na Kadama Malunde
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Msalala kilichojadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Mibako Mabubu, akizungumza wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Msalala cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, akizungumza wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mweka Hazina wa Halmashauri ya Msalala, Daniel Kidana, akisoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Rose Manumba, wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Rose Manumba, akizungumza wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni akiwa kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Msalala cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Na Kadama Malunde - Msalala
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameiomba Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya Ukaguzi Maalum (Special Audit) katika Halmashauri ya Msalala ili kubaini chanzo cha dosari za usimamizi wa fedha zilizoifanya halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka katika ripoti ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mhe. Mhita ametoa maelekezo hayo leo Julai 8, 2026 wakati akizungumza katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa kujadili taarifa ya CAG kuhusu hesabu za halmashauri kwa mwaka wa fedha 2024/2025 baada ya taarifa ya CAG kuwasilishwa na Mweka Hazina wa Halmashauri ya Msalala, Daniel Kidana, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Rose Manumba.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo ni wajibu wa viongozi na watumishi kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa kwa uadilifu na kufika kwa wananchi waliokusudiwa kunufaika.
"Leo mpo kwenye baraza maalumu la kupitia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo Halmashauri ya Msalala imepata hati yenye mashaka. Hili ni jambo ambalo lazima tulitafakari kwa kina," amesema Mhita.
Aidha, Mhita ameeleza kusikitishwa na taarifa za kuwapo kwa mazingira yasiyowezesha wakaguzi wa ndani kutekeleza majukumu yao, ikiwemo kuzuiwa kuingia ofisini na kutokuwepo kwa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya watendaji.
"Halmashauri ya Msalala imekuwa na changamoto za ukaguzi, imekuwa na vuta nikuvute, mkaguzi wa ndani akija anafungiwa mlango asiingie ofisini, mkaguzi wa ndani akija vitasa vya mlango vinavunjwa. Kweli ? Ofisi ya umma? Mnamzuia kuingia?hata mimi Mkuu wa Mkoa siwezi kuzuia Mkaguzi kuingia ofisini kwangu, hii siyo nyumba yangu, ni ofisi ya umma. Lakini Msalala mmejiamini kupitiliza, mmetoka nje ya misingi ya utumishi wa umma, mmeanza kunyanyasana.
Na wakaguzi wote jicho lao ni moja, mkaguzi wa ndani, mkaguzi wa nje wote jicho lao ni moja, kwa hiyo mkaguzi wa ndani atakaposhauri mkachukua kanga mkamfunika kichwani kwamba wewe hufai, atakuja mkaguzi wa nje ataona",ameeleza Mhe. Mhita.
"Mtumishi yule, mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kupitia kwa Katibu Mkuu Barua ikaja mtumishi yule asiondoke kituoni, halmashauri ya Msalala mkakataa maelekezo kutoka TAMISEMI, akaja mtaalamu kutoka ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga ambaye naye amejitahidi sana kwenye hii halmashauri hakupewa ushirikiano. Nayasema haya kwa uchungu mkubwa kwa sababu kazi niliyopewa na Mhe. Rais ni kuja kusimamia utoaji wa huduma kwenye mkoa wa Shinyanga, kuja kuhakikisha nasimamia rasilimali fedha ili ziwafikie wananchi",ameongeza Mhita.
Mhe. Mhita amesema dalili zote zinaonyesha kuwa hoja zilizowahi kutolewa na mkaguzi wa ndani pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa hazikufanyiwa kazi ipasavyo, hali iliyochangia halmashauri kupata hati yenye mashaka.
"Leo hii yale ambayo Mkaguzi wa ndani alikuwa anajaribu kuyaokoa, yale ambayo mtaalamu kutoka ofisi ya RAS alikuwa anajaribu kuyaokoa na mkawaona hawafai yamekuja kuleta hati yenye mashaka. Mkaguzi wa ndani alizungumza kuna changamoto akasimamishwa kazi, mtaalamu wa ofisi ya RAS alikuja hakupata ushirikiano, leo tumepata hati yenye changamoto, hati yenye mashaka",amesema.
"Ili kuepuka kutafuta mchawi, nataka halmashauri hii ipate Special Audit. Naiomba Ofisi ya CAG ifanye ukaguzi maalum ili tujue kinachoendelea katika halmashauri hii na kubaini changamoto za udhibiti na matumizi ya fedha. Wakati huo huo mamlaka zote zinazohusika zifanye ufuatiliaji kwa maslahi ya fedha za wananchi zilizotolewa na Serikali," amesisitiza.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema viongozi wa halmashauri, hususan madiwani, wanapaswa kuwa mstari wa mbele kusimamia matumizi ya fedha za umma na kuhakikisha mifumo ya ukaguzi wa ndani inafanya kazi kwa uhuru na ufanisi.
Ameeleza kuwa tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Mkoa wa Shinyanga umepokea zaidi ya shilingi trilioni 1.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, akisisitiza kuwa fedha hizo zinalenga kutatua changamoto za wananchi na si vinginevyo.
Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe. Mabula Magangila, amesema baadhi ya hoja zilizobainishwa kwenye ripoti ya CAG tayari zimeanza kujibiwa huku nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi.
"Tumepokea ripoti, baadhi ya hoja zimejibiwa na nyingine zinaendelea kujibiwa. Pia tumepokea maelekezo na mapendekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na tutashirikiana kuhakikisha yanatekelezwa," amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Mibako Mabubu, amesema wamepokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na wako tayari kuyatekeleza.
"Tumepokea maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa na tutayafanyia kazi. Tangu halmashauri hii ianzishwe, suala la kupata hati yenye mashaka ni jambo geni. Tulichobaini changamoto kubwa ni upatikanaji wa nyaraka na vielelezo vinavyohitajika," amesema.
Naye Diwani wa Kata ya Isaka, Pazi Majuto, pamoja na Diwani wa Kata ya Bulyanhulu, Musingi Sabaganga, wamesema hati yenye mashaka imetokana na masuala ya kitaalamu yaliyo nje ya uwezo wa madiwani, huku wakiahidi kushirikiana katika utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa.










































Social Plugin