Jeshi la Polisi Tanzania limesema hali ya usalama nchini ni shwari hadi kufikia mchana wa leo, huku likiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudumisha amani na utulivu.
Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP David Misime, baada ya Jeshi hilo kupokea simu nyingi kutoka kwa waandishi wa habari na wananchi wakitaka kufahamu hali ya usalama nchini.
Katika taarifa yake, DCP Misime amesema licha ya leo kuwa ni siku ya mapumziko ya Sikukuu ya Sabasaba, baadhi ya wananchi wameendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii huku hali ya usalama ikiendelea kuwa nzuri.
“Jeshi la Polisi Tanzania linapenda kuwafahamisha Watanzania na wageni waliopo nchini kuwa, hali ya usalama nchini ni shwari,” amesema DCP Misime.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama litaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wakati wote ili kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao kwa amani.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na kujiepusha na matumizi yanayoweza kuvunja sheria, ikiwemo kusambaza taarifa za uongo, kuchochea chuki au kuchonganisha jamii.
DCP Misime amewakumbusha wananchi kuwa kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, hususan Kifungu cha 16 pamoja na sheria nyingine za nchi.

Social Plugin