Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUMIENI MITANDAO KUTAFUTA MASOKO, SI KUKINZANA NA SHERIA– MISIME





Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Katika kipindi ambacho matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku na chachu ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali, Jeshi la Polisi limewataka Watanzania kuitumia teknolojia hiyo kwa busara, maadili na kwa kuzingatia sheria, likionya kuwa matumizi mabaya yanaweza kuhatarisha usalama wa taifa na kuvuruga mshikamano wa jamii.

Akizungumza leo kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP Misime, amesema matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii si tatizo la Tanzania pekee bali ni janga la kidunia linalozikabili nchi nyingi kutokana na uwezo wake wa kusambaza taarifa kwa kasi kubwa, zikiwemo taarifa za upotoshaji, uchochezi na zenye kuhamasisha vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama.

Amesema maendeleo ya teknolojia yameleta fursa nyingi za kiuchumi, elimu na mawasiliano, lakini endapo teknolojia hiyo itatumika vibaya inaweza kuwa chanzo cha migogoro, chuki na kuvunjika kwa mshikamano wa kijamii.

"Mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu sana katika dunia ya leo,tatizo si mitandao yenyewe, bali namna inavyotumiwa. Ikitumika vibaya inaweza kueneza chuki kati ya mtu na mtu, kuchonganisha jamii, kupotosha ukweli na hata kuhatarisha usalama wa nchi.

Hili si tatizo la Tanzania pekee, ni changamoto inayozikabili nchi nyingi duniani," amesema.

DCP Misime amewataka wananchi, hususan vijana ambao ndio watumiaji wakubwa wa mitandao hiyo, kuhakikisha wanachapisha na kusambaza taarifa zenye manufaa kwa jamii badala ya kutumia majukwaa hayo kukiuka sheria au kuhamasisha vitendo vinavyoweza kuleta taharuki na migawanyiko.

Amesema kila Mtanzania ana wajibu wa kutumia uhuru wa kujieleza kwa kuwajibika, akisisitiza kuwa haki hiyo inapaswa kwenda sambamba na kuheshimu sheria za nchi na kulinda amani ambayo imeendelea kuwa msingi wa maendeleo ya taifa.

Akiwa katika viwanja vya Sabasaba, DCP Misime amesema ameshuhudia jinsi wafanyabiashara wengi wanavyotumia mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa na huduma zao, kupata wateja wapya na kuongeza mauzo, jambo linaloonyesha kuwa teknolojia hiyo inaweza kuwa chachu kubwa ya maendeleo ya kiuchumi inapowekewa matumizi sahihi.

"Nimeona wafanyabiashara wengi hapa Sabasaba wakitumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara zao na wanapata matokeo mazuri. Huu ndio mfano tunaopaswa kuufuata,tuitumie teknolojia kujenga uchumi wetu, kuongeza kipato na kuleta maendeleo, badala ya kuitumia kutafuta namna ya kukinzana na sheria au kuleta migawanyiko katika jamii," amesema.

Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii, huku likichukua hatua za kisheria dhidi ya wale watakaotumia majukwaa hayo kufanya uhalifu au kuhatarisha usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa DCP Misime, matumizi yenye uwajibikaji ya mitandao ya kijamii yataendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha uchumi wa kidijitali, kukuza biashara, kuelimisha jamii na kudumisha amani, ambayo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com