Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AJIRA MPYA NI KIPAUMBELE CHA SERIKALI KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI – KIKWETE



Na Veronica Mwafisi-Uyui - Julai 10, 2026

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali inaendelea kuweka ajira mpya kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi, hususan katika sekta za elimu na afya.

Akizungumza leo Julai 10, 2026 katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, kabla ya kukagua na kuzindua Shule ya Msingi Ilolangula Mlimani, Mhe. Kikwete alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta mbalimbali na ndiyo sababu Serikali imeendelea kutoa vibali vya ajira.

Alieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, Serikali imetoa kibali cha kuajiri watumishi 45,000, huku sekta ya elimu ikiwa miongoni mwa zitakazonufaika kwa kiasi kikubwa.

"Serikali inafahamu changamoto ya ajira hususan katika sekta ya elimu na afya. Ndiyo maana Rais wetu amekuwa akiendelea kutoa vibali vya ajira ili kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi," alisema Mhe. Kikwete.

Aidha, alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kupitia ongezeko la watumishi wenye sifa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.

Katika hotuba yake, Mhe. Kikwete aliwahimiza wanafunzi wa Shule ya Msingi Ilolangula Mlimani kusoma kwa bidii, akisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Alisema hata vitabu vitakatifu vya dini vinahimiza umuhimu wa elimu, hivyo wanafunzi wanapaswa kuitumia fursa hiyo kujijengea maarifa yatakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Waziri huyo pia alitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha bajeti inatengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya TAKUKURU katika Wilaya ya Uyui, akieleza kuwa uwepo wa ofisi hiyo utarahisisha mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Mohamed Mtulyakwaku, alieleza kuwa wilaya hiyo bado inakabiliwa na upungufu wa watumishi katika sekta za elimu na afya licha ya Serikali kuendelea kuwapangia watumishi wapya.

Aliiomba Serikali kuendelea kuipa kipaumbele Wilaya ya Uyui katika mgawanyo wa watumishi ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Vilevile, alibainisha kuwa kutokuwepo kwa Ofisi ya TAKUKURU wilayani humo kunawalazimu wananchi na viongozi kusafiri hadi Tabora Mjini kufuata huduma, jambo linaloongeza gharama na usumbufu.

Ziara hiyo ya Uyui imehitimisha rasmi ziara ya kikazi ya siku tatu ya Waziri Ridhiwani Kikwete mkoani Tabora, iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi na watumishi wa umma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com