
Na OWM - TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ametoa wito kwa walimu wote nchini wa shule za awali, msingi na sekondari kufundisha kwa umahiri ili taifa liwe imara na rasilimali watu yenye kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo kwa walimu hao Juni 06, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa shindano la taifa la stadi za ufundishaji kwa walimu wa awali, msingi na sekondari nchini.
“Kaulimbiu hii inayosema Ufundishaji Bora, Taifa Imara ina mashiko, hivyo ninatoa wito kwa walimu mfundisheni vizuri, na wito huu si kwa walimu mlioshinda tu bali ni kwa walimu wote nchi nzima kwani mnapaswa kuzingatia kuwa ufundishaji bora utatupatia taifa imara,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Ili kuwapatia motisha walimu 35 walioshinda katika shindano la taifa la stadi za ufundishaji, Prof. Shemdoe amewaelekeza wakurugenzi wa halmashauri zote ambazo walimu hao wanafundisha kuhakikisha wanawapatia kiwanja ili waendelee kubaki katika vituo vyao vya kazi na kulitumikia taifa, huku viwanja hivyo vikibaki kuwa ni kumbukumbu ya kudumu ya namna Serikali inavyothamini utendaji kazi wao.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amewataka walimu wengi zaidi kujitokeza kushiriki katika shindalo hilo mwakani ili kuibuka washindi na kutambulika kitaifa kutokana na umahiri wao katika stadi za ufundishaji.
Aidha, Prof. Shemdoe amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele kikubwa cha kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu hususani katika eneo la ujifunzaji na ufundishaji, hatua ambayo imeongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema kuwa shindano hilo limejumuisha halmashauri zote 184 za Tanzania Bara na linaratibiwa na Serikali kupitia TET chini ya Programu ya kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) na Mradi wa kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Washindi wa shindano hilo la taifa la stadi za ufundishaji kwa walimu wa awali, msingi na sekondari wamepatiwa zawadi ya fedha tasilimu, kompyuta, kompyuta mpakato, vibao vya kidijitali na projekta kwa ajili ya shule zao ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.











Social Plugin