Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRA SHINYANGA YAADHIMISHA MIAKA 30 YA MLIPAKODI KWA KUFANYA MBIO ZA SHUKRANI NA KUPANDA MITI



Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga imefanya mbio za shukrani za kilometa tano ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA na kuelekea kilele cha Tuzo ya Rais kwa Mlipakodi Bora zinazotarajiwa kufanyika Julai 01, 2026.

Mbio hizo zimefanyika leo Juni 27, 2026 katika Manispaa ya Shinyanga na kushirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya kodi, wakiwemo maafisa usafirishaji na wananchi.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa mbio hizo, Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Maro, amesema tukio hilo limelenga kutoa shukrani kwa walipakodi kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya taifa kupitia ulipaji wa kodi, sambamba na kuhamasisha jamii kuendelea kutimiza wajibu huo kwa hiari.

Amesema ushiriki wa wadau mbalimbali katika mbio hizo unaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya TRA na walipakodi wake, huku akibainisha kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya kodi na huduma bora kwa wateja ili kuongeza uelewa na utii wa sheria za kodi nchini.

Ameeleza kuwa maadhimisho ya miaka 30 ya TRA ni fursa ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo na serikali, pamoja na kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Tanzania.

Kwa upande wake, Mgeni Rasmi katika mbio hizo ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Pendo Sawa, ameipongeza TRA Mkoa wa Shinyanga kwa kuandaa tukio hilo la kuwathamini walipakodi na kuhamasisha ulipaji wa kodi. Amesema walipakodi ndiyo nguzo ya maendeleo ya taifa na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.

Aidha, baada ya zoezi la mbio kukamilika, viongozi na washiriki wa mbio hizo walishiriki upandaji wa miti katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Shinyanga Girls ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

<<<<<TAZAMA PICHA>>>>>




Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Pendo Sawa akiongoza mbio hizo.







Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Maro akizungumza wakati wa zoezi hilo.


Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mhe. Pendo Sawa akizungumza wakati 
wa zoezi hilo.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com