Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TEMESA YAJIVUNIA MAFANIKIO YA MIAKA 20 ,YAAHIDI KUIMARISHA HUDUMA NA MASLAHI YA WATUMISHI WAKE



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) umeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake kwa kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za ufundi, usimamizi wa mitambo pamoja na maboresho ya miundombinu ya umeme nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho hayo iliyofanyika jijini Dodoma June 24,2026 Mkurugenzi Mkuu wa TEMESA Kheri Mahimbali, amesema mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi hicho yametokana na juhudi za wafanyakazi na ushirikiano mzuri kati ya taasisi hiyo, Serikali na sekta binafsi.

Amesema TEMESA imeendelea kupanua wigo wa huduma zake kwa kushirikiana na sekta binafsi, hususan katika maeneo ya matengenezo ya magari, mitambo pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiufundi.

Mahimbali amesema taasisi hiyo imeendelea kuboresha miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo uwekaji na matengenezo ya taa za barabarani, hatua ambayo imechangia kuimarisha huduma kwa wananchi na kuongeza usalama katika maeneo ya mijini na vijijini.

"Tunaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wengine ili kuhakikisha huduma tunazozitoa zinakuwa bora zaidi na zenye tija kwa taifa," amesema.

Amebainisha kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeelekeza taasisi za umma kujiendesha kwa ufanisi na kuongeza tija katika shughuli zake ili ziweze kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa Mahimbali, TEMESA itaendelea kuimarisha shughuli zake za kibiashara ili kuongeza mapato yatakayosaidia kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya watumishi wake.

Aidha, amewapongeza wafanyakazi wa TEMESA kwa mchango wao katika kufanikisha majukumu ya taasisi hiyo kwa kipindi cha miaka 20 na kuahidi kuendelea kushughulikia maslahi yao kwa lengo la kuongeza ari ya kazi na ufanisi katika utoaji wa huduma.

"Nawapongeza watumishi wote wa TEMESA kwa kazi kubwa mnayoifanya kila siku. Uongozi utaendelea kuboresha maslahi yenu ili kuongeza motisha na kuifanya TEMESA izidi kuwa taasisi bora na yenye ushindani," amesema.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com